“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumanne, Desemba 6, 2022
Juma la 2 la Majilio
Isa 40: 1-11;
Zab 95: 1-3, 10-13;
Mt 18: 12-14
MUNGU ANATAFUTA KONDOO ALIYEPOTEA!
Somo la kwanza kutoka katika kitabu cha nabii
Isaya, tunasikia sifa za Mchungaji mwema mwenye huruma na kuwajali kondoo
waliopotea (watu wa Israeli). Katika Injili Yesu anatupa mfano wa kondoo
aliyepotea. Huyu Mchungaji anawaacha wale tisini na tisa na kwenda kumtafuta
aliyepotea. Mfano huu unaendelea na kusema kuwa “atakapo mpata, Amin,
nawaambia, atafurahi zaidi juu ya kondoo huyu, kuliko wale tisini na tisa ambao
hawakupotea” (Mt 18:13). Huzuni na masikitiko ya huyu Mchungaji yanabadilika na
kuwa furaha baada ya kumpata kondoo na kumrudisha kwenye kundi. Kwa haraka
haraka inawezekana kuonekana kama sio sawa kwa Mchungaji kumfurahia zaidi huyu
aliyepotea baada ya kumpata kuliko wale tisini na tisa. Lakini tukitambua
kwamba, kila mmoja wetu ni yule kondoo aliyepotea, ina leta maana zaidi.
Tunapotafakari kuhusu mfano huu ni vizuri kufikiria juu ya hamu na tamaa ya
huyu Mchungaji na jitihada zake za kututafuta. Hii ndio hali ya Mungu juu yetu.
Mungu anatutafuta daima aturudishe kundini mwake.
Tutafakari leo, kuhusu wewe kuwa mmoja wa yule
kondoo aliyepotea. Kupotelea kwenye “dhambi” sio jambo linaloleta furaha,
dhambi inaleta wasi wasi, maumivu, kukosa Amani, kuchanganyikiwa, hasira na
mengine mengi. Lakini tukiinua macho yetu kumwelekea Mchungaji mwema tukiwa
katika hali ya dhambi zetu, tutapata tena matumaini mapya. Tutapata matumaini
kwamba Mungu wetu anatujali na hachoki kamwe kututafuta. Na anapo tupata moyo
wake hujazwa na furaha kuu! Wakati kondoo aliyepotea anapopatikana jumuiya yote
ya mbinguni hufurahi. (Lk 15:7).
Sala: Bwana, katikati ya dhambi zangu na
kuchanganyikiwa nakurudia. Nina amini kwamba unanitafuta. Ninaomba nijiaminishe
kwenye upendo wako wa hali ya juu kwangu. Yesu, nakuamini wewe. Amina
Copyright ©2013-2022 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment