Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, DESEMBA 6, 2022


MASOMO YA MISA, DESEMBA 6, 2022
JUMANNE, JUMA LA  2 LA MAJILIO


SOMO 1
Isa. 40:1 – 11

Watulizeni mioyo, watulizeni mioyo, watu wangu, asema Mungu wenu. Semeni na moyo wa Yerusalemu, kauambieni kwa sauti kuu ya kwamba vita vyake vimekwisha, uovu wake umeachiliwa, kwa kuwa amepokea kwa mkono wa Bwana adhabu maradufu kwa dhambi zake zote.

Sikiliza ni sauti ya mtu aliaye, Itengenezeni nyikani njia ya Bwana, nyosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wetu. Kila bonde litainuliwa, na kila mlima na kilima kitashushwa; palipopotoka patakuwa pamenyoka, na palipoparuza patasawazishwa. Na utukufu wa Bwana utafunuliwa, na wote wenye mwili watauona pamoja, kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena haya.

Sikiliza, ni sauti ya mtu asemaye, Lia! Nikasema, Nilie nini? Wote wenye mwili ni majani, na wema wake wote ni kama ua la kondeni. Majani yakauka, ua lanyauka, kwa sababu pumzi ya Bwana yapita juu yake. Yakini watu hawa ni majani. Majani yakauka, ua lanyauka, bali neon la Mungu wetu litasimama milele.

Wewe uuhubiriye Sayuni habari njema, panda juu ya mlima mrefu; wewe uuhubiriye Yerusalemu habari njema, paza sauti kwa nguvu. Paza sauti yako, usiogope; iambie miji ya Yuda, Tazameni, Mungu wenu! Tazameni, thawabu yake I pamoja naye, na ijara yake I mbele zake. Atalilisha kundi lake kama mchungaji, atawakusanya wanakondoo mikononi mwake; na kuwachukua kifuani mwake, nao wanyonyeshao atawaongoza polepole.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


 
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 96:1 – 3, 10 – 13 (K) Isa. 40:9 – 10

(K) Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa.

Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Mwimbieni Bwana, nchi yote.
Mwimbieni Bwana likarikini jina lake,
Tangazeni wokovu wake siku kwa siku. (K)

Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
Na watu wote habari za maajabu yake.
Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki,
Atawahukumu watu kwa adili. (K)

Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie,
Bahari na ivume na vyote viijazavyo.
Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo,
Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha. (K)

Mbele za Bwana, kwa maana anakuja,
Kwa maana anakuja aihukumu nchi,
Atahukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa uaminifu wake. (K)



SHANGILIO
Aleluya, aleluya,
Siku ya Bwana i karibu, Tazama atakuja kutuokoa.
Aleluya.



INJILI
Mt. 18:12 – 14

Siku ile, Yesu aliwaambia wafuasi wake. Mwaonaje? Mtu akiwa na kondoo mia, mmoja akampotea, je! Hawaachi wale tisa na tisini, akaenda milimani, na kumtafuta yule aliypotea? Hata akipata kumwona, amin, nawaambia, amfurahi huyo Zaidi, kuliko wale tisa na tisini wasiopotea.

Vivyo hivyo haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment