Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, IJUMAA, DESEMBA 23, 2022


MASOMO YA MISA, 
IJUMAA, DESEMBA 23, 2022
JUMA LA 4 LA MAJILIO



SOMO 1
Mal. 3:1 – 4; 4:5 – 6

Bwana Mungu asema: Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi. Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Kwa maana yeye ni mfano wa moto wa mtu asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye nguo; naye ataketi kama asafishaye fkama asafishaye fedha na kuitakasa, naye atawatakasa wana wa Lawi, atawasafisha kama dhahabu na fedha; nao watamtolewa Bwana dhabihu katika haki. Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zitakapopendeza mbele za Bwana, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani.

Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya Bwana, iliyo kuu na kuogofya. Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, ioli nisije nikaipiga dunia kwa laana.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 25:4 – 5, 8 – 10, 14

(K) Changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu unakaribia.

Ee Bwana, unijulishe njia zako,
Unifundishe mapito yako.
Uniongoze katika kweli yako,
Na kunifundisha.
Maana wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu. (K)

Bwana yu mwema, mwenye adili,
Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
Wenye upole atawafundisha njia yake. (K)

Njia zote za Bwana ni fadhili na kweli,
Kwao walishikao agano lake na shuhuda zake.
Siri ya Bwana iko kwao wamchao,
Naye atawajulisha agano lake. (K)


SHANGILIO

Aleluya, aleluya,
Ee Imanueli, Mfalme na Mwanasheria wetu, njoo ukatuokoe, ee Bwana, Mungu wetu.
Aleluya.


INJILI
Lk. 1:57 – 66

Ikawa, siku za kuzaa kwake Elisabeti zilipotimia alizaa mtoto mwanamume. Wakasikia jirani zake na jamaa zake, wakafurahi pamoja naye.

Ikawa siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria. Mamayeakajibu akasema, La, sivyo; bali, ataitwa Yohani. Wakamwambia, Hapana mtu katika jamaa zake aitwaye jina hilo. Wakamwashiria babaye wajue atakavyo kumwita. Akataka kibao, akaandika kwamba, Jina lake ni yohane. Wakastaajabu wote. Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kunena akimsifu Mungu.

Wakaingiwa na hofu wote waliokuwa wakikaa karibu nao; na mambo hayo yote yakatangazwa katika nchi yote ya milima milima ya Uyahudi. Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa namna gani. Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment