MASOMO YA MISA DESEMBA 25, 2022
SHEREHE YA KUZALIWA BWANA
SOMO 1
Isa. 52:7-10
Jinsi ilivyo mizuri juu ya milima, miguu yake aletaye
habari njema, Yeye aitangazaye Amani, aletaye habari njema ya mambo mema, yeye
atangazaye wokovu, auambiaye Sayuni, Mungu wako anamiliki! Sauti ya walinzi
wako! Wanapaza sauti zao, wanaimba pamoja; maana wataona jicho kwa jicho, Jinsi
Bwan arejeavyo Sayuni. Pigeni kelele za furaha, imbeni pamoja, enyi mahali pa
Yerusalemu palipokuwa ukiwa; Kwa kuwa Bwan amewafariji watu wake, Ameukomboa
Yerusalemu. Bwana ameweka wazi mkono wake mtakatifu machoni pa mataifa yote; Na
ncha zote za dunia zitauona wokovu wa Mungu wetu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 98:1-6 (K) 3
(K) Miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. (K)
Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa amedhihirisha haki yake,
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)
Miisho yote ya dunia imeuona,
Wokovu wa Mungu wetu,
Mshangilieni Bwana nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)
Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
Kwa panda na sauti ya baragumu,
Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana. (K)
SOMO 2
Ebr. 1:1 – 6
Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii
kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi
katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya
ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake,
akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi,
aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu; amefanyika bora kupita malaika, kwa
kadiri ya jina alilorithi lilivyo tukufu kuliko lao.
Kwa maana alimwambia malaika yupi wakati wowote, Ndiwe
mwanangu, Mimi leo nimekuzaa? Na tena, mimi nitakuwa kwake baba, Na yeye
atakuwa kwangu mwana? Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema,
Na wamsujudu malaika wote wa Mungu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Aleluya, aleluya!
Siku takatifu imetung’aria: enyi mataifa njoni mkamwabudu
Bwana, kwa sababu leo mwanga mkubwa umeshuka duniani.
Aleluluya.
INJILI
Yn. 1:1-18
Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa
Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote
vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika.
Ndani yake ndimo ulikuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru
yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.
Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake
Yohane. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini
kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru.
Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija
katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata
kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala wali wake
hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu,
ndio wale walioaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi
ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. Naye Neno alifanyika
mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee
atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.
Yohani alimshuhudia, akapaza sauti yake akasema. Huyu
ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Ajaye nyuma yangu amekuwa mbele yangu;
kwa maana alikuwa kabla yangu. Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote
tulipokea, na neema juu ya neema. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa;
neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu
wakati wao wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye
aliyemfunua.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment