Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, DESEMBA 21, 2016


MASOMO YA MISA, DESEMBA 21, 2022
JUMATANO, JUMA LA 4 LA MAJILIO


SOMO 1
Wimb. 2:8 – 14

Sikiliza! Ni mpendwa wangu! Tazama, anakuja akiruka milimani, akichachawa vilimani. Mpendwa wangu ni kama paa, au ayala. Tazama, asimama nyuma ya ukuta wetu, achungulia dirishani, atazama kimiani.

Mpendwa wangu alinena, akaniambia, ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako, maana tazama, kaskazi imepita, masika imekwisha, imekwenda zake; maua yatokea katika nchi, wakati wa kupelea umefika, na sauti ya mwigo husikiwa kwetu. Mtini wapevusha tini zake, na mizabibu inachanua inatoa harufu yake nzuri.

Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako. Hua wangu, mafichoni mwa jabali, katika sitara za magenge, nitazame uso wako, nisikie sauti yako, maana sauti yako ni tamu na uso wako mzuri.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

Au.


Sef. 3:14:14 – 17

Imba, ee binti Sayuni; piga kelele, ee Israeli; furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, ee binti Yerusalemu. Bwana ameziondoa hukumu zako, amemtupa nje adui yako; mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; hutaogopa uovu tena.

Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa, usiogope, ee Sayuni; mikono yako isilegee. Bwana, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa; atakushangilia kwa furaha kuu, atatulia katika upendo wake. Atakufurahia kwa kuimba.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 33:2 – 3, 11 – 12, 20 – 21 (K) 1, 3

(K) Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki: Mwimbieni wimbo mpya.

Mshukuruni Bwana kwa kinubi,
Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.
Mwimbieni wimbo mpya,
Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe. (K)

Shauri la Bwana lasimama milele,
Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi.
Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wako,
Watu aliowachagua kuwa urithi wake. (K)

Nafsi zetu zinamngoja Bwana;
Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
Maana mioyo yetu itamfurahia,
Kwa kuwa tumelitumaini jina lake takatifu. (K)



SHANGILIO
Aleluya, aleluya,
Ee Utokaye Mashariki, uliye mng’ao wa mwanga wa milelel na jua la haki, njoo kuwaangazia wakaao gizani na katika kivuli cha mauti.
Aleluya.



INJILI
Lk. 1:39 – 45

Mariamu aliondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti. Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema,

Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment