MASOMO YA MISA, DESEMBA 19, 2022
JUMATATU, JUMA LA 4 LA MAJILIO
SOMO 1
Amu. 13:2 – 7, 24 – 25
Siku zile, palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya
Wadani; jina lake akiitwa Manoa; na mkewe alikuwa tasa, hakuzaa watoto. Malaika
wa Bwana akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai;
lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume. Basi sasa, jihadhari,
nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi; kwani
tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya
kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye
ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti.
Ndipo yule mwanamke akaenda akamwambia mume wake,
akisema, Mtu wa Mungu alinijia, na uso wake ulikuwa kama uso wa malaika wa
Mungu, wa kutisha sana; nami sikumwuliza, Umetoka wapi? Wala hakuniambia jina
lake; lakini aliniambia, Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume;
basi sasa, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi. Maana
mtoto huyo atakuwa Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni, hata siku ya kufa kwake.
Basi yule mwanamke akamzaa mtoto mwanamume akamwita jina
lake Samsoni, mtoto huyu akakua, Bwana akambarikia. Roho ya Bwana ikaanza
kumtaharakisha katika Mahanedani, katikati ya Sora na Eshtaoli.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 71:3 – 6, 16 – 17 (K) 8
(K) Kinywa changu kitajazwa sifa zako, na heshima yako
mchana kutwa.
Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu,
Uniamuru niokolewe,
Ndiwe genge langu na ngome yangu.
Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi. (K)
Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana Mungu,
Tumaini langu tokea ujana wangu.
Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa,
Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu. (K)
Nitakuja na mambo ya ajabu ya Bwana Mungu,
Nitawakumbusha watu haki yakow ewe peke yako.
Ee Mungu umenifundisha tokea ujana wangu;
Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo. (K)
SHANGILIO
Aleluya, aleluya,
Ee chipukizi la Yese, unayesimama kama ishara ya mataifa,
usikawie kuja kutuokoa.
Aleluya.
INJILI
Lk. 1:5 – 25
Zamani za Herode, mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani
mmoja, jina lake Zakaria, wa zamu ya Abiya, na mkewe alikuwa mmojawapo wa uzao
wa Haruni, jina lake Elisabeti. Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za
Mungu, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama. Nao
walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee
sana.
Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani katika
taratibu ya zamu yake mbele za Mungu, kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura
ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba. Na makutano
yote ya watu walikuwa wakisali nje saa ya kufukiza uvumba. Akatokewa na malaika
wa Bwana, amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia. Zakaria
alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia.
Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana
dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake
utamwita Yohane. Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia
kuzaliwa kwake. Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala
kileo; naye atajazwa roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye. Na wengi
katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao. Naye atatangulia mbele zake
katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee
watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu
waliotengenezwa. Zakaria akamwambia malaika, Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni
mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi. Malaika akamjibu akamwambia, Mimi
ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na
kukupasha habari hizi njema. Na tazama! Utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka
siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo
yatatimizwa kwa wakati wake.
Na wale watu walikuwa wakimngojea Zakaria, wakastaajabia
kukawia kwake mle hekaluni. Alipotoka hali hawezi kusema nao, walitambua ya
kuwa ameona maono ndani ya hekalu, naye aliendelea kuwashiria akakaa bubu.
Ikawa siku za huduma yake zilipokuwa zimetimia akaenda
nyumbani kwake. Hata baada ya siku zile mkewe Elisabeti alichukua mimba akatawa
miezi mitano, akisema, Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana katika siku zile
alizoniangalia ili kuniondolea aibu yangu mbele ya watu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment