MASOMO YA MISA, DESEMBA 18, 2022
DOMINIKA YA 4 YA MAJILIO
WIMBO WA MWANZO: Isa 45:8
Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, mawingu na yammwage
mwenye haki; nchi ifunuke, na kumtoa Mwokozi.
SOMO 1
Isa. 7:10 – 14
Siku zile, Bwana akasema na Ahazi akinena, Jitakie ishara
ya Bwana, Mungu wako; itake katika mahali palipo juu sana. Lakini Ahazi
akasema, Sitaitaka, wala sitamjaribu Bwana.
Naye akasema, Sikilizeni sasa, enyi nyumba ya Daudi; Je!
Ni neno dogo kwenu kuwachosha wanadamu, hata mkataka kumchosha Mungu wangu pia?
Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa
mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli. (Yaani Mungu pamoja nasi.)
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 24:1 – 6 (K) 7, 10
(K) Mfalme mtukufu apate kuingia, Yeye ndiye Mfalme
mtukufu.
Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji aliithibitisha. (K)
Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe.
Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili. (K)
Atapokea Baraka kwa Bwana,
Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. (K)
SOMO 2
Ru. 1:1 – 7
Paulo, mtumwa wa Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume, na
kutengwa aihubiri Injili ya Mungu; ambayo Mungu amekwisha kuiahidi kwa kinywa
cha manabii wake katika maandiko matakatifu.
Yaani, habari za Mwanawe, aliyezaliwa katika ukoo wa
Daudi kwa jinsi ya mwili, na kudhihirishwa kwa uweza kuwa Mwana wa Mungu, kwa
jinsi ya roho ya utakatifu, kwa ufufuo wa wafu, Yesu Kristo Bwana wetu; ambaye
katika yeye tulipokea neema na utume ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa
Imani, kwa ajili ya jina lake; ambao katika hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu
Kristo; kwa wote walioko Rumi, wapendwao na Mungu, walioitwa kuwa watakatifu.
Neema na iwe kwenu na Amani itokayo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu
Kristo.
SHANGILIO
Mt. 1:23
Aleluya, aleluya!
Tazama bikira atachukua mimba, naye atazaa mwana, nao
watamwita jina lake Imanueli: yaani Mungu pamoja nasi.
Aleluya!
INJILI
Mt. 1:18 – 25
Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama
yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba
kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa
haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. Basi alipokuwa akifikiri
hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana
wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho
Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye
atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno
lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii akisema, Tazama, bikira atachukua
mimba, naye atazaa mwana; nao watamwita jina lake Imanueli; yaani, Mungu pamoja
nasi.
Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama
malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment