MASOMO YA MISA, DESEMBA 11, 2022
DOMINIKA YA 3 YA MAJILIO
WIMBO WA MWANZO: Flp 4:4-5
Furahini katika Bwana siku zote; tena nasema furahini.
Bwana yu karibu.
SOMO 1
Isa. 35:1 – 6, 10
Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa
litashangilia na kuchanua maua kama waridi. Litachanua maua mengi, na kufurahi,
naam, kwa shangwe na kuimba; litapewa uzuri wa Lebanoni, utukufu wa Karmeli na
Sharoni; watauona utukufu wa Bwana, ukuu wa Mungu wetu. Itieni nguvu mikono
iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea.
Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope;
tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa
ninyi.
Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi
yatazibuliwa. Ndipo mtu aliye kilema atarukaruka kama kulungu, na ulimi wake
aliye bubu utaimba. Na hao waliokombolewa na Bwana watarudi, watafika Sayuni
wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko
na furaha, huzuni na kuugua zitakimbia.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 146:6 – 10 (K) Isa. 35:4
(K) Uje Bwana kutuokoa.
Huishika kweli milele.
Huwafanyia hukumu walioonewa,
Huwapa wenye njaa chakula;
Bwana hufungua waliofungwa. (K)
Bwana huwafumbua macho waliopofuka;
Bwana huwainua walioinama;
Bwana huwapenda wenye haki;
Bwana huwahifadhi wageni. (K)
Huwategemeza yatima na mjane;
Bali njia ya wasio haki huipotosha.
Bwana atamiliki milele,
Mungu wako, Ee Sayuni, kizazi hata kizazi. (K)
SOMO 2
Yak. 5:7 – 10
Ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima
hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata
yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho. Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo
yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia. Ndugu, msinung’unikeane, msije
mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango. Ndugu, watwaeni
manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa
uvumilivu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Lk. 4:18
Aleluya, aleluya,
Roho wa Bwana yu juu yangu, amenituma kuwahubiri maskini
habari njema.
Aleluya.
INJILI
Mt. 11:2 – 11
Siku ile, Yohane aliposikia huko gerezani matendo yake
Kristo, alituma wanafunzi wake, kumwuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie
mwingine? Yesu akajibu akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohane mnayoyasikia na
kuyaona; vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa,
viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema. Naye
heri awaye yote asiyechukizwa nami.
Na hao walipokwenda zao, Yesu alianza kuwaambia makutano
habari za Yohane, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini? Unyasi ukitikiswa na
upepo? Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa mavazi mororo? Tazama,
watu wavaao mavazi mororo wamo katika nyumba za wafalme. Lakini kwa nini
mlitoka? Ni kuona nabii? Naam, nawaambia, na aliye mkuu zaidi ya nabii. Huyo ndiye
aliyeandikiwa haya, Tazama mimi namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako,
Atakayeitengeneza njia yako mbele yako.
Amin, nawaambieni, Hajaondokea mtu katika wazao wa
wanawake aliye mkuu kuliko Yohane Mbatizaji; walakin aliye mdogo katika ufalme
wa mbinguni ni mkuu kuliko yeye.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment