Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

KITAMBULISHO CHA KUINGIA KATIKA UFALME WA MUNGU!


“MBEGU ZA UZIMA”
Jumapili, Desemba 11, 2022 
Dominika 3 ya Majilio

Isa 35:1-6, 10;
Zab 145:6-10; 
Yak 5:7-10; 
Mt.11:2-11.


KITAMBULISHO CHA KUINGIA KATIKA UFALME WA MUNGU!

Jumapili ya tatu ya Majilio inajulikana kama Dominika ya Gaudete au Dominika ya furaha. Hii ni kwasababu Antifona ya misa, inatualika “tufurahi katika Bwana daima, na tena tufurahi kwasababu Bwana yupo karibu” (Flp 4:4-5). Neno Gaudete ni neno la kilatini lenye maana "furahi". Majilio kuwa kipindi cha kujiandaa kwa ujio wa Masiha (ujio wake kwa Noeli na ujio wake katika Maisha yajayo), kwa jumapili ya tatu ya majilio tupo nusu ya kipindi cha majilio, na hivyo kuna haja ya kufurahi tunapoona lengo letu linakaribia “Bwana yu Karibu”. 

Nabii Isaya anaanza kwa unabii kwamba sehemu ya jangwa litafurahi na kuimba na litasitawi kwa maua mengi. Kwasababu “watauona utukufu wa Bwana, na ukuu wa Mungu wetu”. Somo linaendelea kwa kujenga nguvu na kutia moyo kwamba: “Mungu wetu anayekuja atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu, atakuja na kuwaokoa ninyi. Ndipo mtu aliye kilema ataruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba. Na hao waliokombolewa na Bwana watarudi, watafika Sayuni wakiimba. Na hao waliokombolewa na Bwana watarudi, watafika Sayuni wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; na watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua zitakimbia”.

Somo la pili kutoka katika barua ya Yakobo 5:7-10 linatuhabarisha tuwe wavumilivu mpaka Bwana atakapo kuja. Yakobo anatuambia tuwe na uvumilivu kama ule wa Mkulima anaeyengojea mazao yake. Mkulima huvumilia tangu “mvua ya kwanza hadi ya mwisho”. Anatutia moyo na nguvu “tuwe na uvumilivu kwani Bwana yu karibu”.

Injili kutoka kwa Mwinjili Mathayo leo ina sehemu mbili. Kwanza kabisa, Yohane Mbatizaji, yupo gerezani na anawatuma wanafunzi wake kwa Yesu kumuuliza “Wewe ndiye yule ajaye au tumtazamie mwingine? Yesu anawatuma wamwambie Yohane walichosikia na walichoona “vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa habari njema.”  Na anaendelea kusema *Naye heri yeyote asiyechukizwa nami”. Katika sehemu ya pili ya Injili, wakati wale waliotumwa na Yohane wakijiandaa kwenda, Yesu anamsifia Yohane Mbatizaji kwa kuwauliza umati maswali mbali mbali juu ya walienda jangwani kutazamani nini?. Yesu anathibitisha kwamba ni kweli walienda kumuona nabii , “naam, zaidi ya nabii”. Anafafanua kwanini Yohane ni zaidi ya nabii; yeye ndiye aliyetimiza ujumbe wa nabii Malaki 3:1, ambapo ujumbe husema “tazama mimi  namtuma mjumbe wangu mbele ya uso wako atakayeitengeneza njia yako mbele yako.” Na mwisho kabisa Yesu anasema kwamba “Amin, nawaambieni hajaondokea mtu katika uzao wa wanawake aliye mkuu kama Yohane mbatizaji; lakini aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yeye.

Wayahudi katika kipindi hicho cha siku za Yesu, walikuwa na mawazo juu ya Masiha atakuwaje na atafanya nini. Ilikuwa kawaida kudhani kuwa Masiha atakuwa kama Wafalme wa dunia ambaye atawaokoa na utawala wa Kirumi uliokuwa ukichukiwa , walidhani Masiha atawasaidia kupindua utawala huo kwa nguvu za kijeshi. Yohane Mbatizaji huwenda akawa alishirikishwa pia mawazo na matarajio kama haya, pamoja na kwamba alikuwa amepokea ufunuo unaomuelekeza kumuonesha Yesu kama Mwana-kondoo wa Mungu. (Yn 1:30-34). Kuliko kupoteza Imani, Yohane aliona bora kuwatuma wafuasi wake ili kuondoa wasi wasi, kama hali hiyo Masiha ni sahihi au la. Yesu anaelekeza kwamba Yeye ndiye Masiha wa Kweli. Akionesha kwamba ametimiza miujiza yote ilioandikwa (kama inayooneshwa katika somo la kwanza) na kutangaza habari njema sawa sawa na kipindi cha Masiha.

Wakati wale wajumbe wa Yohane wakiondoka, Yesu anatoa heshima kwa mkuu wao, akieleza kwamba Yohane alikuwa nabii wa kweli-na zaidi ya nabii-alikuwa ni mjumbe aliyetabiriwa na nabii Malaki, kuwa atamtambulisha Masiha. Hili linamfanya kuwa nabii mkuu zaidi ya wote, ndio maana Yesu alisema katika uzao wa wanawake hajatokea mkuu kama Yohane Mbatizaji. Licha ya hili Yesu anasema kwamba “mdogo katika Ufalme wa Mungu” ni mkuu kuliko yeye. Katika hali hii, Ufalme wa Mungu katika hali ya kidunia kama Kanisa, katika kipindi cha Ukristo, ambapo Yohane hakuuishi muda huu. Hivyo kila Mkristo-mwanaume, Mwanamke- mtoto- amebarikiwa zaidi kuliko Yohane kwasababu sisi tunashiriki katika Ufalme wa Kristo tukiwa hapa duniani kama Kanisa, huku tukisubiria ukamilifu wake wakati ujao. Sisi tunamuishi Kristo na kubahatika kuishi ujumbe wake aliotangaza, kushiriki katika neema zake nyingi, na kuwa sehemu ya Mwili wa fumbo la Kristo yaani Kanisa. 

Je, sio bahati sisi kuwa sehemu ya Ufalme wa Yesu, Masiha ? sio bahati kushiriki katika baraka za kuwa sehemu ya mwili wa Kristo? Ndio ni bahati. Lakini pia katika maisha yetu ya kila siku, tunatambua mapungufu yetu, tumekuwa watu wakufuata dhambi zaidi bila kufuata utukufu, tunaopenda huzuni zaidi kuliko furaha. Liturjia ya leo inatujaza tena nguvu na furaha kwamba Bwana wetu yupo karibu. Tunaitwa tuijongee sakramenti ya kitubio, tutubu, kwa kufanya maungamo mazuri. Tujitafiti kuhusu utakaso ambao Mungu anatuitia. Ni kitu gani kinachotuzuia kuona neema ya Mungu ambacho Yesu anataka tukiachie/ukiachie? Tujikabizi katika moto wa Upendo wa Mungu uweze kututakasa na tuache upendo huo ututakase katika “jumapili hii ya furaha” na katika kipindi chote cha majilio na maisha yetu yote.

Sala: Bwana, ninatamani roho yangu itakaswe nawe. Ninatamani utakatifu wa maisha. Naomba unisaidie nianze hali hii mara moja, ili nianze kufurahia furaha na uhuru uliouweka ndani mwangu. Yesu nakuamni wewe. Amina.

                                     
Copyright ©2013-2022 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment