Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, NOVEMBA 8, 2022


MASOMO YA MISA, NOVEMBA 8, 2022
JUMANNE, JUMA LA 32 LA MWAKA WA KANISA

SOMO 1
Tit. 2:1 – 8, 11 – 14

Wewe nena mambo yapasayo mafundisho yenye uzima; ya kwamba wazee wawe wenye kiasi, wastahivu, wenye busara, wazima katika Imani na katika upendo na katika saburi. Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema; ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao; na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe.

Vivyo hivyo na vijana waume uwaonye kuwa na kiasi; katika mambo yote ukijionyesha wewe mwenyewe kuwa kielelezo cha matendo mema, na katika mafundisho yako ukionyehsa usahii na ustahivu, na maneno yenye uzima yasiyoweza kuhukumiwa makossa, ili yule mwenye kupinga atahayarike, kwa kuwa hana neno baya la kunena juu yetu.

Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katiak ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye Baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 37:3 – 4, 18, 23, 27, 29 (K) 39

(K) Wokovu wa wenye haki una Bwana.

Umtumaini Bwana ukatende mema,
Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu.
Nawe utajifurahisha kwa Bwana,
Naye atakupa haja za moyo wako. (K)

Bwana anazijua siku za wakamilifu,
Na urithi wao utakuwa wa milele.
Hatua za mtu zaimarishwa na Bwana,
Naye aipenda njia yake. (K)

Jiepue na uovu, utende mema,
Na kukaa hata milele.
Wenye haki watairithi nchi,
Nao watakaa humo milele. (K)


SHANGILIO
Zab. 119:18

Aleluya, aleluya,
Unifumbue macho yangu niyatazame maajabu yatokayo katika sheria yako.
Aleluya.


INJILI
Lk. 17: 1-10

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ni nani kwenu mwenye mtumwa alimaye au auchungaye ng’ombe, atakayemwambia mara arudipo kutoka shambani, Njoo upesi, keti, ule chakula? Je! Hatamwambia, Nifanyie tayari chakula, nile; jifunge unitumikie, hata niishe kula na kunywa, ndipo nawe utakapokula na kunywa? Je! Atampa asante yule mtumwa, kwa sababu ameyafanya aliyoagizwa? Vivyo hivyo nayi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.



Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment