MASOMO YA MISA, NOVEMBA 7, 2022
JUMATATU, JUMA LA 32 LA MWAKA WA KANISA
SOMO 1
Tit. 1:1 – 9
Paulo, mtumwa wa Mungu, na mtume wa Yesu Kristo; kwa
ajili ya Imani ya wateule wa Mungu, na ujuzi wa kweli ile iletayo utauwa;
katika tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu asiyeweza kusema uongo aliuahidi
tangu milele; akalifunua neno lake kwa majira yake katika ule ujumbe
niliowekewa amana mimi kwa amri ya Mwokozi wetu Mungu; kwa Tito, mwanangu hasa
katika Imani tuishirikiyo. Neema na iwe kwako na amani zitokazo kwa Mungu Baba
na kwa Kristo Yesu Mwokozi wetu.
Kwa sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze
yaliyopunguka, na kuweka wazee katika kila mji kama vile nilivyokuamuru; kiwa
mtu hakushitakiwa neno, naye ni mume wa mke mmoja, ana watoto waaminio,
wasioshitakiwa kuwa ni wafisadi wala wasiotii. Maana imempasa askofu awe mtu
asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni wakili wa Mungu; asiwe mtu wa kujipendekeza
nafsi yake, asiwe mwepesi wa hasira, asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda
mapato ya aibu; bali awe mkaribishaji, mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki,
mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake; akilishika lile neno la Imani vile vile
kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na
kuwashinda wenye kupinga.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 24: 1 – 6 (K) 6
(K) Hiki ndicho kizazi cha wakutafutao, Ee Bwana.
Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji aliithibitisha. (K)
Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,
Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili. (K)
Atapokea Baraka kwa Bwana,
Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. (K)
SHANGILIO
1Sam. 3:9, Yn. 6:68
Aleluya, aleluya,
Nena, Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia: wewe unayo
maneno ya uzima wa milele.
Aleluya.
INJILI
Lk. 17:1 – 6
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Makwazo hayana budi kuja,
lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake! Ingemfaa zaidi mtu huyo
jiwe la kusaga lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kulikko kumkosesha
mmojawapo wa wadogo hawa. Jilindeni.
Kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama
akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema,
Nimetubu, msamehe.
Mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee Imani. Bwana akasema,
Kama mngekuwa na Imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu,
Ng’oka ukapandwe baharini, nao ungewatii.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment