Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA NOVEMBA 29, 2022


MASOMO YA MISA NOVEMBA 29, 2022
JUMANNE , JUMA LA 1 LA MAJILIO


SOMO 1
Isa. 11:1-10

Siku ile litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda. Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa nay a kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawanya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya. Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia.

Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kimono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza. Ng’ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng’ombe. Na mtoto anyonayaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira. Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari.

Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzika patakuwa na utukufu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 72:1-2,7-8,12-13,17 (K) 7

(K) Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi na wingi wa Amani kwa milele.

Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako,
Na mwana wa mfalme haki yako
Atawaamua watu wako kwa haki,
Na watu wako walioonewa kwa hukumu. (K)

Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi,
Na wingi wa Amani hata mwezi utakapokoma.
Na awe na enzi toka bahari hata bahari,
Toka Mto hata miisho ya dunia. (K)

Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo,
Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi,
Atamhurumia aliye dhaifu na maskini,
Na nafsi za wahitaji ataziokoa. (K)

Jina lake na lidumu milele,
Pindi ling’aapo jua jina lake liwe na wazao;
Mataifa yote na wajibariki katika yeye,
Na kumwita heri. (K)



SHANGILIO
Aleluya, aleluya,
Tazama Bwana wetu atakuja na nguvu, na atayaangaza macho ya watumishi wake.
Aleluya.



INJILI
Lk. 10:21-24

Siku ile, Yesu alishangilia kwa Roho Mtakatifu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu nan chi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote ambaye Mwana apenda kumfunulia.

Akawageukia wanafunzi wake, akasema nao kwa faragha, Heri macho yaonayo mnayoyaona ninyi. Kwa kuwa nawaambia ya kwamba manabii wengi na wafalme walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi wasiyasikie.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment