Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, NOVEMBA 26, 2022


MASOMO YA MISA, NOVEMBA 26, 2022
JUMAMOSI, JUMA LA  34 LA MWAKA WA KANISA


SOMO 1
Ufu. 22:1 – 7

Malaika alinionyesha, mimi Yohane, mto wa maji ya uzima, wenye kung’aa kama bilauri, aukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwanakondoo, katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa. Wala hapatakuwa na laana yoyote tena. Na kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwanakondoo kitakuwamo ndani yake. Na watumwa wake watamtumikia; nao watamwona uso wake, na jina lake litakuwa katika vipaji vya nyuso zao. Wala hapatakuwa na usiku tena; wala hawana haja ya taa wala ya nuru ya jua; kwa kuwa Bwana Mungu huwatia nuru, nao watatawala hata milele na milele.

Kisha akaniambia, Maneno haya ni amini na kweli. Naye Bwana, Mungu war oho za manabii, alimtuma malaika wake kuwaonyesha watumwa wake mambo ambayo hayana budi kuwako upesi. Na tazama, naja upesi; heri yeye ayashikaye maneno ya unabii wa kitabu hiki.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 95:1 – 7 (K) 1Kor. 16:22, Ufu. 22:20

(K) Maranatha, Uje, Bwana Yesu.

Njoni tumwimbie Bwana,
Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
Tuje mbele zake kwa shukrani,
Tumfanyie shangwe kwa zaburi. (K)

Kwa kuwa Bwana ni Mungu mkuu,
Na mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Mkononi mwake zimo bonde za dunia.
Hata vilele vya milima ni vyake.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya,
Na mikono yake iliiumba nchi kavu. (K)

Njoni, tuabudu, tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake. (K)



SHANGILIO
Zab. 119:135

Aleluya, aleluya,
Umwangazie mtumishi wako uso wako, na kunifundisha amri zako.
Aleluya.



INJILI
Lk. 21:34-36

Yesu aliwambia wanafunzi wake: Jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo; kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima. Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika hayo yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment