MASOMO YA MISA, NOVEMBA 29, 2024
IJUMAA, JUMA LA 34
LA MWAKA WA KANISA
SOMO 1
Ufu. 20:1 – 4, 11 – 21:2
Mimi, Yohane, niliona malaika akishuka kutoka mbinguni,
mwenye ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa mkononi mwake. Akamshika yule
joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu;
akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akamtia muhuri juu yake, asipate
kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa
afunguliwe muda mchache.
Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao
wakapewa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda
wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala
sanamu yake, wala hawakuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala
katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu.
Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, nay eye
aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao
hapakuonekana. Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho
kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho
ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika
vile vitabu, sawasawa na matendo yao.
Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na
Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri
ya matendo yake. Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo
mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. Na iwapo mtu yeyote hakuonekana
ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.
Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana za
kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena. Nami
nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa
Mungu, umewekwa tayari, kama bibi arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 84:2 – 5, 7 (K) Ufu. 21:3
(K) Mungu anakuwa pamoja na watu.
Nafsi yangu imeziona shauku nyua za Bwana,
Naam, na kuzikondea.
Moyo wangu na mwili wangu
Vinamlilia Mungu aliye hai. (K)
Shomoro naye ameona nyumba,
Na mbayuwayu amejipatia kioto,
Alipoweka makinda yake, kwenye madhabau zako,
Ee Bwana wa majeshi,
Mfalme wangu na Mungu wangu. (K)
Heri wakaao nyumbani mwako,
Wanakuhimidi daima.
Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako,
Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake. (K)
SHANGILIO
Zab. 19:8
Aleluya, aleluya,
Amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru.
Aleluya.
INJILI
Lk. 21:29-33
Yesu aliwaambia wanafunzi wake mfano, Utazameni mtini na
miti mingine yote. Wakati iishapo kuchipuka, mwaona na kutambua wenyewe ya
kwamba majira ya mavuno yamekwisha kuwa karibu. Nanyi kadhalika, mwonapo
yamekwisha kuwa karibu. Nanyi kadhalika, mwonapo mambo hayo yanaanza kutokea,
tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu u karibu. Amin, nawaambieni, Kizazi hiki
hakitapita hata hayo yote yatimie. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu
hayatapita kamwe.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment