Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, NOVEMBA 23, 2022


MASOMO YA MISA, NOVEMBA 23, 2022
JUMATANO, JUMA LA 34 LA MWAKA WA KANISA


SOMO 1
Ufu. 15:1 – 4

Mimi, Yohane, niliona ishara nyingine katika mbingu, iliyo kubwa, naya ajabu; malaika saba wenye mapigo saba ya mwisho; maana katika hayo ghadhabu ya Mungu imetimia. Tena nikaona kitu kama mfano wa bahari ya kioo iliyochangamana na moto, wa wale wenye kushinda, watokao kwa yule mnyama, na sanamu yake, na kwa hesabu ya jina lake, walikuwa wamesimama kandokando ya hiyo bahari ya kioo, wenye vinubi vya Mungu. Nao wauimba wimbo wa Musa, mtumwa wa Mungu, na wimbo wa Mwanakondoo, wakisema.
Ni makuu, naya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi; Ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa. Ni nani asiyekucha, Ee Bwana, na kulitukuza jina lako? Kwa kuwa wewe peke yako u Mtakatifu; kwa maana mataifa yote watakuja na kusujudu mbele zako; kwa kuwa matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 98:1 – 3, 7 – 9 (K) Ufu. 15:3

(K) Matendo yako ni makuu, Ee Bwana Mungu Mwenyezi.

Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. (K)

Bwana ameufunua wokovu wake,
Machozi pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)

Bahari na ivume na vyote viijazavyo,
Ulimwengu nao wanaokaa ndani yake.
Mito na ipige makofi,
Milima na iimbe pamoja kwa furaha. (K)

Mbele za Bwana;
Kwa maana anakuja aihukumu nchi.
Atauhukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa adili. (K)



SHANGILIO
1Thes. 2:13

Aleluya, aleluya,
Lipokeeni neno la Mungu, siyo kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu.
Aleluya.



INJILI
Lk. 21:12-19

Yesu aliwaambia wanafunzi wake; Watawakamata na kuwaudhi; watawapeleka mbele ya masinagogi, na kuwatia magerezani, mkipelekwa mbele ya wafalme na maliwali kwa ajili ya jina langu. Na hayo yatakuwa ushuhuda kwenu. Basi, kusudieni mioyoni mwenu, kutofikirifikiri kwanza mtakavyojibu; Kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga. Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawafisha baadhi yenu. Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu. Walakini hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu. Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment