Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, NOVEMBA 21, 2022


MASOMO YA MISA, NOVEMBA 21, 2022
JUMATATU, JUMA LA 34 LA MWAKA WA KANISA

KUTOLEWA BIKIRA MARIA HEKALUNI


SOMO 1
Zek. 2:10 – 13

Imba, furahi, Ee binti Sayuni; maana, tazama, anakuja, nami nitakaa, kati yako, asema Bwana. Na mataifa mengi watajiunga na Bwana katika siku ile, nao watakuwa watu wangu; nami nitakaa kati yako, nawe utajua ya kuwa Bwana wa majeshi amenituma kwako. Na Bwana atairithi Yuda, iwe sehemu yake katika nchi takatifu, naye atachagua Yerusalemu tena. Nyamazeni, ninyi nyote wenye mwili, mbele za Bwana; kwa maana ameamka, na kutoka katika maskani yake takatifu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Lk. 1:46 – 55 (K) 49

(K) Mwenye nguvu amenitendea makuu, na jina lake ni takatifu.

Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,
Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu. (K)

Kwa kuwa ameutazama
Unyonge wa mjakazi wake.
Kwa maana, tazama, tokea sasa
Vizazi vyote wataniita mbarikiwa;
Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu,
Na jina lake ni takatifu. (K)

Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi
Kwa hao wanaomcha.
Amefanya nguvu kwa mkono wake;
Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao. (K)

Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi;
Na wanyonge amewakweza.
Wenye njaa amewashibisha mema,
Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu. (K)

Amemsaidia Israeli, mtumishi wake;
Ili kukumbuka rehema zake;
Kama alivyowaambia baba zetu,
Ibrahimu na uzao wake hata milele. (K)



SHANGILIO
Lk. 1:28

Aleluya, aleluya,
Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Umebarikiwa katika wanawake.
Aleluya.



INJILI
Lk. 11:27 – 28

Yesu aliposema maneno hayo, mwanamke mmoja katika mkutano alipaza sauti yake, akamwambia, Heri tumbo lililokuzaa, Afadhali, heri walisikiao neno la Mungu na kulishika.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment