Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA NOVEMBA 20, 2022


MASOMO YA MISA NOVEMBA 20, 2022
JUMAPILI YA MWISHO WA MWAKA C 

SHEREHE YA BWANA WETU YESU KRISTU MFALME



WIMBO WA MWANZO: Ufu. 5:12;1-6

Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima.
Utukufu na ukuu una yeye hata milele na milele.



SOMO 1
2Sam. 5:1 -3

Ndipo kabila zote za Israeli wakamwendea Daudi huko Hebroni, wakasema naye, wakinena, Tazama, sisi tu mfupa wako na nyama yako. Zamani za kale, hapo Sauli alipokuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyewaongoza Israeli watoke nje, na kuingia ndani. Naye Bwana akakuambia, Wewe utawalisha watu wangu Israeli, nawe utakuwa mkuu juu ya Israeli. Basi, wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni; naye mfalme Daudi akapatana nao huko Hebraoni mbele za Bwana; wakamtia Daudi mafuta awe mfalme juu ya Israeli.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 122:1 – 5 (K) 1

(K) Nalifurahi waliponiambia, na twende nyumbani kwa Bwana.

Nalifurahi waliponiambia,
Na twende nyumbani kwa Bwana.
Miguu yetu imesimama,
Ndani ya malango yako Ee Yerusalemu. (K)

Ee Yerusalemu uliyejengwa,
Kama mji ulioshikamana;
Huko ndiko walikopanda kabila,
Kabila za Bwana. (K)

Ushuhuda kwa Israeli,
Walishukuru jina la Bwana.
Maana huko huko viliwekwa viti vya hukumu,
Viti vya enzi vya nyumba ya Daudi. (K)



SOMO 2
Kol. 1:11 – 20

Mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu pamoja na furaha; mkimshukuru Baba, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru. Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi.

Naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana, ikiwa ni viti vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliubwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hukshikana katika yeye. Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote. Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake, akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



INJILI
Lk. 23:35 – 43

Watu walisimama wakitazama Yesu. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake. Wale askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki, huku wakisema, Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe. Na juu yake palikuwa na anwani: HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI.

Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi. Lakini yule wa pili akamjibu, akamkemea akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tulivyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lolote lisilofaa. Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.



Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment