Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, NOVEMBA 17, 2022


MASOMO YA MISA, NOVEMBA 17, 2022
ALHAMISI, JUMA LA 33 LA MWAKA WA KANISA

KUMBUKUMBU YA MT. ELIZABETI WA HUNGARIA (MTAWA)


SOMO 1
Ufu. 5:1 – 10

Mimi, Yohane, niliona katika mkono wa kuume wake yeye  aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi, kitabu kilichoandikwa ndani na nyumba, kimetiwa muhuri saba. Nikaona malaika mwenye nguvu akihubiri kwa sauti kuu, N’nani astahiliye kukifungua kitabu, na kuzivunja muhuri zake? Wala hapakuwa na mtu mbinguni,  wala juu ya nchi, wa la chini ya nchi, aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama. Nami nikalia sana kwa kuwa hapakuonekana mtu astahiliye kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama. Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye aliye na kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba.

Nikaona katikati ya kiti cha enzi na wale wenye uhai wane, na katikati ya wale wazee, Mwanakondoo amesimama, alikuwa kana kwamba amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, ambazo ni Roho saba za Mungu zilizotumwa katika dunia yote. Akaja, akakitwaa kile kitabu katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi. Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wane na wale wazee ishirini na wane wakaanguka mbele za Mwanakondoo, kil ammoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya watakatifu.

Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 149:1 – 6, 9 (K) Ufu. 5:10

(K) Ulitufanya kuwa wafalme na makuhani.

Aleluya.
Mwimbieni Bwana mwimbo mpya,
Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
Israeli na amfuhie Yeye aliyemfanya,
Wana wa SAyuni na wamshangilie mfalme wao. (K)

Na walisifu jina lake kwa kucheza,
Kwa matari na kinubi wamwimbie.
Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake,
Huwapamba wenye upole kwa wokovu. (K)

Watauwa na waushangilie utukufu,
Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wake wote.
Aleluya. (K)



SHANGILIO
Yn. 17:17

Aleluya, aleluya,
Neno lako ndiyo kweli, Ee Bwana, ututakase kwa ile kweli.
Aleluya.



INJILI
Lk. 19:41-44

Yesu alipofika karibu ya Yerusalemu aliuona mji, akaulilia, akisema, Laiti ungalijua, hata wewe, katika siku hii, yapasayo Amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako. Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.



Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment