MASOMO YA MISA, NOVEMBA 15, 2022
JUMANNE, JUMA LA 33 LA MWAKA WA KANISA
SOMO 1
Ufu. 3:1 – 6, 14 – 22
Mimi Yohane, nilisikia Bwana anayeniambia: Kwa malaika wa
kanisa lililoko Sardi andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na hizo Roho saba
za Mungu, na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa
hai, nawe umekufa. Uwe mwenye kukesha, ukayaimarishe, ukayaimarishe mambo
yaliyosalia, yanayotaka kufa. Maana sikuona matendo yako kuwa yametimilika
mbele za Mungu wangu.
Basi kumbuka jinasi ulivyopokea, na jinsi ulivyosikia;
yashike hayo na kutubu. Walakini usipokesha, nitakuja kama mwivi, wala hutaijua
saa nitakayokuja kwako. Lakini unayo majina machache katika Sardi, watu
wasioyatia mavazi yao uchafu. Nao watakwenda pamoja nami hali wamevaa mavazi
meupe, kwa kuwa wamestahili. Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala
sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake
mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake. Yeye aliye na sikio, na alisikie
neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.
Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; haya
ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Sahahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa
kuumba kwa Mungu. Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto;
ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu,
wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. Kwa kuwa
wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya
kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.
Nakupa shauri, ununu kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa
moto, upate kuwa tajiri; na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako
usionekane; na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona. Wote
niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidi, ukatubu. Tazama,
nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango,
nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.
Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti
changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika
kiti chake cha enzi. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho
ayaambia makanisa.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 15:1 – 4 (K) Ufu. 3:21
(K) Yeye ashindaye, nitamketisha pamoja nami.
Bwana, ni nani atakayekaa
Katika hema yako?
Ni mtu aendaye kwa ukamilifu,
Na kutenda haki. (K)
Asemaye kweli kwa moyo wake,
Asiyesingizia kwa ulimi wake.
Wala hakumtenda mwenziwe mabaya.
Wala hakumsengenya jirani yake.
Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa,
Bali huwaheshimu wamchao Bwana. (K)
Hakutoa fedha yake apate kula riba,
Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia.
Mtu atendaye mambo hayo hataondoshwa milele. (K)
SHANGILIO
Lk. 8:15
Aleluya, aleluya,
Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao,
hulisikia neno la Mungu, na kulishika.
Aleluya.
INJILI
Lk. 19:1-10
Yesu alipoingia Yeriko alipita katikati yake. Na tazama,
palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni
tajiri. Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa
sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo. Akatangulia mbio, akapanda juu
ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile.
Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu,
akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani
mwako. Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha. Hata watu
walipoona, walinung’unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi.
Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa
maskini, na ikiwa nimenyang’anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne. Yesu
akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa
Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment