Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

HUKUMU YA HAKI/MATUMAINI YA MAISHA YAJAYO!


“MBEGU ZA UZIMA”
JUMAPILI, NOVEMBA 13, 2022
DOMINIKA YA 33 YA MWAKA C WA KANISA

Mal 4:1-2
Zab 98:5-9, (k) 9
2The. 3:7-12
Lk 21:5-19

HUKUMU YA HAKI/MATUMAINI YA MAISHA YAJAYO!

Katika somo la Kwanza tunaowaona Waisraeli baada ya kurudi utumwani Babeli, wanaanza kujisahau tena nakurudia matendo maovu alama ya kumsahau Mungu. Mungu anamtuma nabii Malaki awakumbushe ya kwamba Bwana atakuja na atawahukumu wale wote ambao hawaifuati sheria yake. Wale ambao hawaifuati sheria ya Bwana watakuwa kama makapi. Ndugu zangu sisi nasi tunakumbushwa kwamba uovu daima unatuweka mbali na Mungu na kwamba siku ya hukumu yetu tusipokuwa safi hatutakuwa na kibali mbele ya macho ya Mungu. Sisi tunatambua siku ya mwisho wa maisha yetu tutahukumiwa na Mungu kadiri ya matendo yetu. Tukibaki katika muunganiko na Mungu tukiwa tunamtumaini yeye, hofu na mashaka na wasi wasi vitaondoka. Kama tunavyosikia ahadi ya wale wanolitii na kulicha jina la Bwana, nabii Malaki anasema “jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika mbawa zake”. Hii ndio ahadi ya Mungu kwa wale wanao litii jina la Bwana kila wakati bila kuchoka.

Mara nyingi tunashawishika kumwacha Mungu na hata wakati mwingine tunajikuta tukiridhika tuu na hali yetu ya dhambi tukijiona au tukifikiri kuwa muda bado wa kuishi. Kipindi hiki cha mwisho mwisho cha mwaka wa Lirtujia masomo yanatukumbusha tena, tujichunguze tuangalie uhusiano wetu na Mungu kama upo sawa sawa. Tujitafiti tuingie ndani kabisa mwa mioyo yetu tuangalie ni kitu ghani au ni kikwazo ghani kina nifanya nikose neema ya Mungu moyoni mwangu? Je, ni tamaa ya fedha mnoo, inanifanya nihangaike mpaka nisahau kabisa kumkumbuka Mungu? Je, mali yangu imekuwa kipao mbele kiasi cha kusahau nafasi ya kwanza ambayo ni nafasi ya Mungu? Ni kitu ghani kinapoteza uhusiano huu wangu na Mungu? Je, ni starehe? Tujitafiti kweli kweli bila kujihurumia na kuamua sasa kusimika upya ule upendo wa Mungu aliouweka kwetu kwa njia ya Kristo. Turudishe tena lile tumaini jipya aliloliweka Kristo wakati wa ubatizo wetu. Tuwashe tena ule mwanga wa mshumaa uliokuwa ukiwaka tulipo batizwa, kile kitambaa cheupe tulichowekewe kichwani kama alama ya usafi wa moyo, tukiangalie tena kama kimechafuka tukioshe kwa sakramenti ya kitubio. Tusiridhike na dhambi zetu. Dhambi zinatuweka mbali na Mungu na zinafuta matumaini ya furaha ya maisha ya jayo.
Daima tukifanya haya tusisahau kuwa hakuna mtu anaweza kuwa Mkristo mwenyewe. Daima tunasonga mbele tukiwa tumeshikana mikono pamoja kama wana wa Mungu. Kutafuta wokovu wako mwenyewe tu, bila kuwasaidia walio karibu nao au ndugu zako haiwezi kuleta maana sana na pengine si baraka kama hutujitahidi kuwasaidia na kuwarudisha ndugu zetu katika njia ilio sawa.

Katika somo la pili tunamsikia Mtume Paulo akiwaagiza Wathesalonike wajishughulishe kufanya kazi. Kati ya jambo ambalo liliwatesa Wathesalonike ilikuwa nikuhusu ujio wa pili wa Bwana wetu Yesu Kristo. Wao walidhani siku hiyo ipo karibu sana na daima walijibidisha kujianda wakidhani ni siku Fulani na tarehe Fulani? Walisubiri sana, mpaka pale walipoelewa alichosema Yesu kwamba “hakuna aijuaye siku wala saa” na pia walisahua Yesu alisema kesheni kila wakati kwani siku hiyo itawajia kama Mwivi. Hali hii ya kusubiri ujio wa Kristo iliwafanya Wathesalonike waache kufanya kazi kwasababu wao waliona ya nini kufanya kazi wakati Kristo anakuja kutuchukua? Ndio maana leo Paulo anawasihi wafanye kazi na anawaambia asiyefanya kazi na asile. Paulo alitaka kuwaambia kwamba kukesha katika kumsubiri Kristo katika maisha ya Mkristu aitupasi kufikiri kuwa kufanya kazi ni kazi bure. Kama wanadamu ni lazima kufanya kazi tujipatie riziki zetu za kila siku. Katika nyakati zetu pengine sisi angekuja Paulo angetuambia tumefanya kazi mno kiasi cha kumsahau Mungu. Tumejitafutia riziki yetu na hata baada ya kupata tunatafuta zaidi ili tujiwekee akiba ya baadaye, huku tukidhani kuwa tunaweza kutegemeza wakati ujao kwa vitu vingi tulivyo navyo. Tumekuwa na vingi kiasi cha kutupelekea kuwa wachoyo na kushindwa kuwashirikisha wengine. Pengine riziki zetu alizotupa Mungu zimekuwa chanzo cha majivuno yetu na kushindwa kuona tena thamani ya mwanadamu mwenzangu. Pengine tumezama ndani ya riziki hizi anazo tupa Mungu kiasi cha kusahau umuhimu wa kukumbuka maisha yajayo. Pengine tunafurahia na kuzama ndani yake na kujidanganya kwamba maisha ni hapa duniani tu hamna maisha mengine.

Ndugu zangu leo Paulo anataka kutufundisha kwamba kila mara tunapotafuta riziki zetu, tujue na tutambue kwamba hata kama tungefanikiwa vipi au tungetajirika vipi, nafasi ya Mungu katika maisha yetu ipo pale pale. Tukijaliwa riziki iwe ndio njia njema zaidi ya kujifunza kuwa wakarimu. Pia katika hali nyingine tusidhani kwamba baada ya kuwa na Imani na Kristo na kushika maagizo yake, napaswa kujitenga na wenzangu au kujitenga na kuacha kufanya kazi ya kupata mahitani ya Mwili. Miili ni muhimu kwa ajili ya wokovu wa roho zetu, unatumia mwili wako kusali na kuneemesha roho, ni lazima tufanye kazi bila kusahau nafasi ya Mungu ili tuweze kupata riziki ambayo tutaitumia kuilishia miili yetu. Sisi ni wanadamu tulio na roho na mwili, mwili ni hekalu la roho anamokaa Mungu, ni lazima kuipenda miili yetu pia na kuifanya safi, bila kusahau mwili huu tunapaswa tuutumie vizuri ili tuweze kuifikisha roho yetu katika lile tumaini la Kristo alilo tuandalia.

Ndugu zangu katika Kristo, kati ya mambo yanayo muogopesha mwanadamu ni kifo. Na najaribu kujiuliza kama mwanadamu angejua anakufa siku Fulani, pengine angeweza kufa hata kabla ya siku yenyewe kwasababu ya hofu na mahangaiko. Lakini leo Yesu anataka kutuambia katika Injili kwamba sisi wana wake tunaposikia juu ya mwisho wa maisha yetu au mwisho wa dunia, haitupasi kuogopa kwani Kristo yupo daima pamoja nasi. Lililo jema na jema kabisa ni kujiweka tayari daima kwani tukifanya hivyo tutaziponya nafsi zetu kama Kristo anavyosema mwishoni mwa Injili. Anatupa angalisho katika kuenenda katika tumaini lake kwamba, yapo majaribu mengi sana na misukosuko mingi, yapo mafundisho ya uongo na manabii wa uongo watakao kuja na kutuyumbisha juu ya Imani yetu. Yesu anatufundisha tubaki imara. Tusiyumbishwe na kupepetwa katika Imani yetu tuliopokea kwake na kwa njia ya mitume tunaendelea nayo mpaka sasa.

Katika kuenenda katika matumaini ya maisha yajayo tunapaswa kufanya yafuatayo: Kusali daima. Ili kuondoa wasi wasi na hofu ni lazima kumtumainia Mungu daima na kutambua kuwa, hata kama watu wote watakukimbia na kukutenga ujue kuna mmoja anaye kusikiliza naye ni Mungu. Hii ni kwasababu watu wengine huweza kuhalalisha dhambi kwa kigezo kwamba sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. Lakini si kila mara sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. Wakati hakuna wakukusikiliza tambua yupo mmoja anayekusikiliza, naye ni Mungu. Wakati ukiwa mpweke na huna wakukufariji, tambua daima Mungu yupo karibu na watu wake.

Jambo jingine katika kutumaini ni katika mateso jifunze daima kubaki katika njia ya Imani na daima baki katika jambo la kwanza ambalo ni sala. Mateso ni sehemu ya maisha ya mwanadamu lakini ni lazima kufanya kila jitihada kupunguza na kuondoa mateso. Tunaweza kuyapunguza na kuyaondoa kwa muda mateso lakini tutambue hatuwezi kuyaondoa kabisa mateso yasiwepo tena. Kuteseka na wanao teseka na kuteseka kwasababu ya ukweli na haki, kuteseka kwasababu ya upendo, na ili kuwa mtu unayependa katika kweli-hizi ni sifa za mwanadamu na kusema kuziondoa hizi ni sawa na kumwondoa mwanadamu mwenyewe. Kumbuka kuwaombea wale ambao pengine kwa namna moja au nyingine unatambua ni chanzo cha mateso yako. Katika kusali waombee Baraka ya Mungu ili awabadilishe, usiwaombee mabaya. Kwahiyo matendo yetu na mateso katika maisha yetu tutambue vipo lakini isiwe chanzo cha kuiacha Imani yangu.

Jambo jingine la mwisho, katika kutumaini ni kuhusu hukumu ya Mungu. Tutambue kuwa haki ya Mungu haipingani na neema au huruma yake. Mungu mwenyewe anaweza kuitengeneza haki na Imani inatupa hakika ya hilo. Kuangalia hukumu ya mwisho kama hali ya kutisha na kujijengea ishara za kutisha tutapoteza matumaini. Tusijitengenezee alama za Mungu na kumwekea sifa ambazo si zake. Kujijengea taswira ya Mungu anayehukumu kwa ukali kabisa na Mungu anayeadhibu tuu, pengine inaweza kutujengea dhamira ya woga na hofu ya kushindwa kutumainia huruma ya Mungu pale tunapomkosea. Sisi tutambue Mungu yupo tayari kutusamehe, na kati ya kitu ambacho Mungu hawezi kuacha kusamehe ni moyo wa unyenyekevu uliojishusha kwake na kuomba msamaha. Moyo wenye majivuno na usiopenda kutubu na kumrudia ni dhahiri kwamba ni vigumu kupata huruma ya Mungu. Tunapaswa tutazame hukumu ya mwisho kama alama ya matumaini. Mungu ni haki na hutengeneza haki, na katika haki yake kuna neema.

Mwisho kabisa katika safari yetu ya matuamiani, Bikira Maria aliye nyota ya bahari ambaye hutuliza mawimbi ya bahari. Tusichoke kumwendea na kumwomba atuombee kwa mwanae neema za kusafiri nasi ili tuweze kuvuka bahari ya machafuko salama, na kupata taji la maisha yetu katika maisha yajayo.

Tunapokaribia kufunga mwaka wa Huruma ya Mungu jumapili ijayo,ujumbe wa leo unatualika kujiandaa wenyewe kuishi mwaka huu tulio uadhimisha daima. Kuna watu ulimwenguni na wengine pembeni yetu wanaoteseka sana, wanao onewa, waliokataliwa na wengine wanateseka kwasababu ya majanga mbali mbali. Je, tutawaoneshaje huruma hawa watu? Njia pekee ya kuwasaidia ni kuwapa ujumbe wa matumaini ambao neno la Mungu linatuambia leo.

Sala: Ee Bwana wa matumaini yote, tuongoze vyema tuweze kustahili kuingia katika furaha yako. Amina.

Copyright ©2013-2022 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

No comments:

Post a Comment