ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumatano, Oktoba 30, 2024
Juma la 30 la Mwaka wa Kanisa
Efe 6:1-9;
Zab 144:10-14;
Lk 13:22-30
MLANGO WAKUINGIA KATIKA UFALME WA MUNGU!
Mungu ametuandalia maisha ya uzima wa milele na maisha haya ni kwa ajili ya wote. Yesu anasema katika Injili ya leo, “Nao watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu” (Lk 13:29). Kitu kimoja ambacho ni hakika ni kwamba hakuna upendeleo katika Ufalme wa Mungu. Petro anatuambia katika Kitabu cha matendo ya Mitume, “kwa hakika ninajua Mungu hana upendeleo, bali katika kila taifa anayemuogopa yeye nakufanya yalio haki anakubaliwa naye. (Mdo10:34-35). Hivyo yule mtu alivyo muuliza Yesu, “je ni wachache watakao okolewa ?”. Yesu hakumjibu moja kwa moja. Yesu hasemi ni wachache au wengi, hawa au wale, anasema tu “jitahidini kuingia katika mlango mwembamba” . (Lk 13:23-24). Kwahiyo kwa kadiri ya Yesu ni kwa wale wanaojitahidi kuingia kupitia mlango huo watakao ingia.
Na kwasababu mlango wa kuingia katika uzima wa milele ni mwembamba, waweza kujichunguza ni mizigo mingapi uliobeba ambayo yaweza kukuzuia kuingia, usije kukumbwa na mshangao. Yesu anasema “Na tazama, wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho” (Lk 13:30). Walioteuliwa waweza kuwa wa mwisho. Watu kutoka kaskazini na kusini, magharibi na Mashariki waweza kuwatangulia. Kwahiyo, wale wanaodhani wana nafasi ya pekee katika Ufalme wa Mungu kwasababu tuu wana elimu kuhusu Yesu, au kwasababu wanaenda kanisani kila jumapili, au kwasababu wamesikia mahubiri ya kila jumapili wasije wakashangaa ikawa kinyume. Hili ndilo onyo la Yesu. Kwa njia nyingine tuangalie sana kama kila tunalotenda ni kwa ajili ya ufalme wa Mungu na kumrudishia yeye utukufu au ni kwa ajili ya utukufu binafsi? Manake twaweza kufanya yote vyema ili tuonekane machoni pa watu na kusifiwa na wanadamu, tukajijengea utukufu binafsi! Kwa njia hii tusishangae siku ya mwisho.
Sala: Bwana Yesu, asante kwa zawadi ya ukombozi. Naomba unipe neema ili niweze kuwa miongoni mwao wote watakao okolewa nawe nakuingia katika Ufalme wako. Amina.
Copyright
©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment