Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, OKTOBA 26, 2022


MASOMO YA MISA, OKTOBA 26, 2022
JUMATANO, JUMA LA 30 LA MWAKA WA KANISA

SOMO 1
Efe. 6:1 – 9

Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki. Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia. Nanyi, akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana.

Enyi watumwa, watiini wao walio bwana zenu kwa jinsi ya mwili kwa hofu na kutetemeka, kwa unyofu wa moyo, kana kwamba ni kumtii Kristo; wal asi kwa utumwa wa macho tu kama wajipendekezao kwa wanadamu; bali kama watumwa wa Kristo, mkitenda yampendezayo Mungu kwa moyo; kwa nia njema kama kumtumikia Bwana wala si mwanadamu; mkijua ya kuwa kila neno jema alitendalo mtu atapewa lilo hilo na Bwana, kwamba ni mtumwa au kwamba ni huru.

Nanyi, akina bwana, watendeeni wao yayo hayo, mkiacha kuwaogofya, huku mkijua ya kuwa yeye aliye Bwana wao na wenu yuko mbinguni, wala kwake hakuna upendeleo.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 145:10 – 14 (K) 10

(K) Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru.

Ee Bwana kazi zako zote zitakushukuru,
Wacha Mungu wako watakuhimidi,
Wataunena utukufu wa ufalme wako,
Na kuuhadithia uweza wako.
Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu,
Na utukufu wa fahari ya ufalme wake. (K)

Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote. (K)

Bwana huwategemeza wote waangukao,
Huwainua wote walioinama chini. (K)



SHANGILIO
1Sam. 3:9 Yn. 6:68

Aleluya, aleluya,
Nena Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia, wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya.



INJILI
Lk. 13:22 – 30

Yesu alikuwa akipita katika miji na vijiji, akifundisha, katika safari yake kwenda Yerusalemu. Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaokolewa katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia wasiweze.

Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako; ndipo mtakapoanza kusmea, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu. Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu.

Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje. Nao watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu.

Na tazama, wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.                        

No comments:

Post a Comment