Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, OKTOBA 30, 2022


MASOMO YA MISA, OKTOBA 30, 2022
DOMINIKA YA 31 YA MWAKA

SOMO 1
Hek. 11:22 – 12:2

Ulimwengu wote mbele zako Bwana, ni kama chembe moja katika mizani, na mfano wa tone moja la umande lishukalo asubuhi juu ya ardhi. Lakini Wewe unawahurumia watu wote, kwa sababu unao uweza wa kutenda mambo yote; nawe wawaachilia wanadamu dhambi zao, ili wapate kutubu. Kwa maana Wewe wavipenda vitu vyote vilivyopo, wala hukichukii kitu chochote ulichokiumba. Kwa kuwa hungalifanya kamwe kitu chochote kama ungalikichukia; tena kitu chochote kingaliwezaje kudumu, ila kwa mapenzi yako? Au kitu kisichoumbwa nawe kingaliwezaje kuhifadhika? Lakini Wewe unaviachilia vyote, kwa kuwa ni vyako, Ee Mfalme Mkuu, mpenda roho za watu; maana roho yako isiyoharibika imo katika vyote. Kwa hiyo wawathibitishia kidogo kidogo hatia yao, wale wanaokengeuka kutoka katika njia njema; wawaonya, ukiwakumbusha kwa mambo yale yale wanayokosa, ili waokoke katika ubaya wao, na kukuamini Wewe, Bwana.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 145:1 – 2, 8 – 11, 13 – 14 (K) 1

(K) Ee Mungu Mfalme wangu, Nitalitukuza jina lako milele.

Ee Mungu wangu, Mfalme, nitakutukuza,
Nitalihimidi jina lako milele na milele.
Kila siku nitakuhimidi,
Nitalisifu jina lako milele na milele. (K)

Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma,
Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema,
Bwana ni mwema kwa watu wote.
Na rehema zi juu ya viumbe vyake vyote. (K)

Ee Bwana, viumbe vyako vyote vitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Waunena utukufu wa ufalme wako.
Na kuuhadithia uweza wako. (K)

Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote.
Bwana huwategemeza wote waangukao,
Huwainua wote walioinamia chini. (K)

SOMO 2
2Thes. 1:11 – 2:2

Kwa hiyo twawaomba ninyi sikuzote, ili Mungu wetu awahesabu kuwa mmekustahili kuitwa kwenu, akatimiza kila haja ya wema na kila kazi ya Imani kwa nguvu; jina la Bwana wetu Yesu litukuzwe ndani yenu, nanyi ndani yake, kwa neema ya Mungu wetu nay a Bwana wetu Yesu Kristo.
Basi, ndugu, tunakusihini, kwa habari ya kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, na kukusanyika kwetu mbele zake, kwamba msifadhaishwe upesi hata kuiacha nia yenu, wala msisitushwe, kwa roho, wala kwa neno, wala kwa waraka unaodhaniwa kuwa ni wetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

SHANGILIO
Lk. 2:36

Aleluya, aleluya,
Kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kusimama mbele za Mwana wa Adamu.
Aleluya.

INJILI
Lk. 19:1 – 10

Yusu alipoingia Yeriko alipita katikati yake. Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri. Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo. Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile. Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako. Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha. Hata watu walipoona, walinung’unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi. Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang’anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne. Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo. 


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.                        

No comments:

Post a Comment