Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, IJUMAA, OKTOBA 14, 2022


MASOMO YA MISA, 
IJUMAA, OKTOBA  14, 2022
JUMA LA 28 LA MWAKA


Efe 1:11-14

Ndani yake kristo sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake. Nasi katika huyo tupatane kwa sifa ya utukufu wake sisi tulio tangulia kumwekea Kristo tumaini letu. Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, habari njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye mtakatifu. Ndiye aliye arabuni ya urithi wenu, ili kuleta ukombozi wa milli yake, kuwa sifa ya utukufu wake.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu


WIMBO WA KATIKATI
Zab 33:1-2, 4-5, 12-13

(K) Heri Taifa, Mungu aliowachagua kuwa urithi wake.

Mpigieni Bwana vigelegele enyi wenye haki
Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo
Mshukuruni bwana kwa kinubi
Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa (K)

Kwa kuwa neno la Bwana lina adili
Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu
Huzipenda haki na hukumu
Nchi imejaa fadhili za Bwana (K)

Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao
Watu waliochaguliwa kuwa urithi wake
Toka mbingu bwana huchungulia
Huwatazama wanadamu wote pia (K)


SHANGILIO
Zab 147:12-15

Aleluya , aleluya
Msifuni bwana, Ee Yerusalemu
Huipeleka amri yake juu ya nchi
Aleluya.


INJILI
Lk. 12:1-7

Wakati huo, makutano walipokutanika elfu elfu, hata wakakanyagana, alianza kuwaambia wanafunzi wake kwanza, Jilindeni na chachu ya Mafarisayo, ambayo ni unafiki. Lakini hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa, wala lililofichwa ambalo halitajulikana. Basi, yoyote mliyosema gizani yatasikiwa mwangani; na mliyonena sikioni mwa mtu katika vyumba vya ndani, yatahubiriwa juu ya dari.

Name nawaambia ninyi rafiki zangu, msiwaogope hao wauuao mwili, kisha baada ya hayo hawana wawezalo kutenda Zaidi. Lakini nitawaonya mtakayemwogopa, mwogopeni yule ambaye akiishakumwua mtu ana uweza wa kumtupa katika Jehanam; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo. Je! Mashomoro watano hawauzwi kwa senti mbili? Wala hasahauliwi hata mmojawapo mbele za Mungu. Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi, bora ninyi kuliko mashomoro wengi.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment