“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumatatu, Julai 29, 2024
Juma la 17 la Mwaka
KUMBUKUMBU YA FAMILIA WA MARTA, MARIA NA LAZARO
Yer 13:1-11;
Kum 32: 18-21;
Yn 11: 19-27 or Lk 10: 38-42
NGUVU YA YESU DHIDI YA MAUTI!
“Yesu aliwapenda, Martha, Maria na Lazaro” (Yn 11: 5). Maneno haya ya pekee katika Injili ya Yohane yanatueleza juu ya uhusiano wa pekee aliokuwa nao Yesu kati ya Martha, Maria na Lazaro. Inaonekana Yesu alikuwa mgeni wao mara nyingi katika familia hii huko Bethania, kijiji kidogo, maili mbili kutoka mji wa Yerusalemu. Tunasoma safari tatu za Yesu anazofanya ili kuwatembelea, katika Injili ya Luka 10:38-42, Yn 11: 1-53, Yn 12: 1-9. Sisi nasi tujenge Upendo kama huo na Yesu, mwana wa Mungu, tumjue Mungu. Tunaomba yeye asiwe tu mgeni wetu kila Mara katika maisha bali awe sehemu ya kiini cha familia zetu.
Wakati Yesu alipowatembelea mara ya pili, Martha alikuwa akiomboleza na kulia juu ya kifo cha Lazaro kaka yake, na nyumba ikiwa imejawa pia na waombolezaji wengine. Lakini aliposikia Yesu amefika mahali pale, anasimama mara na kuwaacha wageni wengine na waombolezaji na anaenda kumuona Yesu. Hapa tunamuona Martha aliyebadilika. Pamoja na kwamba yupo katika hali ya majonzi na uchungu anaenda kumuona Yesu. Sasa anatambua lililo muhimu katika maisha. Katika mazungumzo yake anaanza moja kwa moja bila kuwa na wasi wasi kwamba anaamini juu ya nguvu ya Yesu, katika ufufuo wa wafu. Kwasababu ya hili analeta usemi uliomaarufu sana katika Injili ya Yohani. “MIMI (Yesu) ni ufufuo na uzima; aniaminiye mimi, hata kama anakufa ataishi na anayeishi na kuniamini hatakufa kamwe”. Baada ya hili, Martha analeta tena ungamo la Imani “ndio Bwana, ninaamini wewe ni Masiha , Mwana wa Mungu, ajaye ulimwenguni”. Na sasa Yesu anamfufua Lazaro.
Kwa njia hii tunamuona Martha anavyoshirikiana na Neema ya Mungu katika maongezi yake na Yesu, sisi nasi tumpe Yesu nafasi aongee na sisi, sala zetu zisiwe ni sisi tu tunaongea na kueleza mambo yetu pekee, bali tumruhusu pia Mungu aongee nasi. Tumpe pia Mungu nafasi ajibu maombi yetu. Tuwe na muda wa kutafakari katika ukimya tumsikilize Mungu anataka kusema nini juu yangu? Tuwe na muda pia wa kumshukuru sio kuomba tuu, sala yetu iwe na nyanja mbali mbali. Tuwe na muda wa kumsifu, kumshukuru, kumuomba, kumsikiliza na pia kutafakari juu ya ukuu wake, na zaidi sana juu ya upendo aliotuonesha kupitia kwa Mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwanjia yake watu wote wapo hai.
Sala: Bwana, nina amini kwamba utanifufua siku ya mwisho, nizaliwe katika maisha ya umilele. Amina.
Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment