MASOMO YA MISA, JULAI 29, 2024
JUMATATU, JUMA LA 17 LA MWAKA
KUMBUKUMBU YA FAMILIA WA MARTA, MARIA NA LAZARO
SOMO 1
Yer. 13:1-11
Bwana aliniambia hivi, Enenda, ukajinunulie mshipi wa kitani, ukajivike viuno, wala usiutie majini. Basi nikanunua mshipi sawasawa na neno la Bwana, nikajivika viunoni. Nalo neno la Bwana likanijia mara ya pili, kusema, Twaa mshipi ule ulioununua, ulio viunoni mwako, kisha ondoka, enenda mpaka mto Frati, ukaufiche huko katika pango la jabali. Basi nikaenda, nikauficha karibu na mto Frati, kama Bwana alivyoniamuru.
Hata ikawa baada ya siku nyingi, Bwana akaniambia, Ondoka, enenda mpaka mto Frati, ukautwae ule mshipi, niliokuamuru kuuficha huko. Ndipo nikaenda mpaka mto Frati, nikachimba, nikautwaa ule mshipi katika mahali pale nilipouficha; na tazama, mshipi ulikuwa umeharibika, haukufaa tena kwa lo lote. Ndipo neno la Bwana likanijia, kusema, Bwana asema hivi, Jinsi iyo hiyo nitakiharibu kiburi cha Yuda, na kiburi kikuu cha Yerusalemu. Wata hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wanaokwenda kwa ushupavu wa mioyo yao, na kufuata miungu mingine ile kuitumikia na kuiabudu, watakuwa hali moja na mshipi huu, usiofaa kwa lo lote. Maana kama vile mshipi unavyoshikamana na viuno vya mtu, ndivyo nilivyowashikamanisha nami nyumba yote ya Israeli, na nyumba yote ya Yuda, asema Bwana; wapate kuwa watu kwangu mimi, na jina, na sifa, na utukufu; lakini hawakutaka kusikia.
Neno la Mungu...Tumshukuru Mungu
WIMBO WA KATIKATI
Kum. 32:18-21 (K) 18
(K) Humkumbuki Mwamba aliyekuzaa.
Humkumbuki Mwamba aliyekuzaa.
Mungu aliyekuzaa umemsahau.
Bwana akaona, akawachukia,
Kwa sababu ya kukasirishwa na wanawe na binti zake. (K)
Akasema, Nitawaficha uso wangu,
Nitaona mwisho wao utakuwaje;
Maana, ni kizazi cha ukaidi mwingi,
Watoto wasio imani ndani yao. (K)
Wamenitia wivu kwa kisicho Mungu,
Wamenikasirisha kwa ubatili wao;
Nami nitawatia wivu kwa wasio watu.
Nami nitawakasirisha kwa taifa lipumbaalo. (K)
SHANGILIO
Kol. : 16,17
Aleluya, aleluya, Neno la Kristu likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkimshukuru Mungu Baba kwa Yeye. Aleluya.
INJILI
Yn. 11:19 – 27
Watu wengi katika Wayahudi walikuwa wamekuja kwa Martha na Mariamu, ili kuwafariji kwa habari ya ndugu yao. Basi Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alikwenda kumlaki; na Mariamu alikuwa akikaa nyumbani. Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. Lakini hata sasa najua ya kuwa yoyote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa. Yesu akamwambia, Ndugu yako atafufuka. Maratha akamwambia, Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho.
Yesu akamwambia, Mimi ndimi ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo?
Akamwambia, Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Au
INJILI
Lk. 10:38 – 42
Ikawa katika kuenenda kwao aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake. Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake. Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie. Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2024 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment