MASOMO YA MISA, JULAI 10, 2024
JUMATANO, JUMA LA 14 LA MWAKA WA KANISA
SOMO 1
Hos. 10:1 – 3, 7 – 8, 12
Bwana asema hivi: Israeli ni mzabibu, utoao matunda yake; kwa kadiri ya wingi wa matunda yake; kwa kadiri iyo hiyo ameongeza madhabahu zake; kwa kadiri ya wema wan chi yake, kwa kadiri hiyo hiyo wamefanya nguzo nzuri. Moyo wao umegawanyika; sasa wataonekana kuwa na hatia; yeye atazipiga madhabahu zao, ataziharibu nguzo zao. Yakini sasa watasema, Hatunamfalme; kwa maana hatumchi Bwana; na mfalme huyu je! Aweza kututendea nini? Katika habari za Samaria, mfalme wake amekatiliwa mbali, kama povu usoni pa maji. Israeli, pataharibika; mwiba na mbigili itamea juu ya madhabahu zake; nao wataiambia milima, Tusitirini; na vilima, tuangukeni. Jipandieni katika haki, vuneni kwa fadhili; uchimbueni udongo wa mashamba yenu; kwa maana wakati umewadia wa kumtafuta Bwana, hata atakapokuja na kuwanyeshea haki.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 105:2 – 7 (K) 4
(K) Siku zote mtafuteni uso wake Bwana.
Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi,
Zitafakarini ajabu zake zote.
Jisifuni kwa jina lake takatifu,
Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana. (K)
Mtakeni Bwana na nguvu zake,
Utafuteni uso wake sikuzote.
Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya.
Miujiza yake na hukumu za kinywa chake. (K)
Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake;
Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu;
Duniani mwote mna hukumu zake. (K)
SHANGILIO
2 Tim. 1:10
Aleluya, aleluya,
Mwokozi wetu Yesu Kristo alibatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika kwa Injili.
Aleluya.
INJILI
Mt. 10:1 – 7
Yesu aliwaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya; Wa kwanza Simoni aliyeitwa Petro, na Andrea nduguye; Yakobo wa Zebedayo, na Yohane nduguye; Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru; Yakobo wa Alfayo, na Thadayo; Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote, naye ndiye mwenye kumsaliti. Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema.
Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wowote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kodnoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2024.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment