“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumanne, Julai, 9, 2024
Tafakari ya kila siku
Juma la 14 la Mwaka wa Kanisa
Hos 8: 4-7, 11-13;
Zab 115: 3-10;
Mt 9: 32-38
WATETEA IMANI!
Tukijaribu kufikiria kuhusu mpangilio na muunganiko ulivyo katika Kanisa Katoliki, tukijaribu kurudi tangu mwanzo wa kipindi cha mitume, mafundisho yake, msimamo wake, tamaduni zake zinazoletea faraja, sakramenti mbali mbali, umoja wa mafundisho yake, uongozi wa asili ya mitume, mpangilio wake katika kazi ya watakatifu na mashahidi, liki neemeshwa na naombezi ya Mama wa Bwana wetu Yesu Kristo, tukitizama pia umoja wa uwepo wa Mkombozi wetu juu ya Altare, tunajisikia Kanisa hili, Moja, Takatifu, Katoliki la Mitume limetupatia mpangilo mzuri sana na kuwa jua linalo angaza kuondoa giza.
Ni hakika, tangu mwanzoni kabisa Kanisa limepingana kwa hali zote na mafundisho ya uongo yaliojaribu kuharibu ujumbe halisi wa mapokeo ya Mitume. Kanisa limebaki aminifu na litaendelea kubaki aminifu kwa kiini cha mafundisho ya Imani juu ya Kristo.
Sisi pia mara nyingi tumekutana na watu wengi wanaotuuliza maswali kuhusu Imani yetu, na zaidi sana kuhusu kumhesimu Bikira Maria na kumuomba atuombee na pia kuhusu watakatifu au kuhusu sakramenti na zaidi sana sakramenti ya Kitubio na mengine mengi. Huwa tunakabiliano nao vipi? Leo Injili inatufundisha jinsi ya kukabiliana na hali hizo katika maisha yetu.
Injili inatuambia kwamba, mara nyingi Yesu aliwaonea huruma wale wasiokuwa na msaada, walioteseka na wale waliotengwa. Watu mashuhuri hawakupenda Yesu awape nafasi ya kwanza wadhambi na kula pamoja nao. Lakini Yesu hakuwasikiliza walivyo mlaumu. Kama Yesu tunapaswa kuwa imara tunapotaka kuyumbishwa juu ya Imani yetu na tunu za Injili. Kanisa Katoliki sio Kanisa la Biblia tu, lina Mapokeo Matakatifu (mafundisho ya mitume na mababa wa Kanisa, Mafundisho ya Mababa watakatifu n.k), bahati mbaya au kwakutotaka kuyafahamu wengi wanao uliza maswali haya, hawayajui na zaidi sana hawapo tayari kujifunza kwasababu kwao kama kitu hakijaandikwa kwenye Biblia sio kitu kizuri. Kanisa Katoliki chanzo cha mafundisho yake yamejikita katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo Matakatifu (Sacred Tradions), kwahiyo Kanisa Katoliki sio dini ya Biblia tu. Tunapaswa kuwa Makini kuhusu Imani yetu, tusiyumbishwe , tushikilie imara kile tunacho amini, mafundisho yalio asili ya Imani yetu.
Najaribu kufikiria hivi wale wanaokataa mapokeo, je mapokeo sio matokeo pia ya kusoma Biblia? Hivi wao wanapofafanua Biblia, je, maneno wanayo tumia kufafanua yameandikwa kwenye Biblia? Maneno wanayohubiri Mtu akiyaandika na baadae akaja kuwafundisha watu je sio mapokeo ambayo yametokana na mtu kusoma Biblia? Ukikataa Mapokeo maana yake umekataa pia watu wasifafanue Biblia kwani, utakavyo fafanua lazima utatumia maneno yako kueleza na ni hakika yatakuwa hayajaandikwa kwenye Biblia. Ni ngumu sana kukataa Mapokeo. Ukikataa mapokeo uwe tayari kuwaambia watu kwamba nikusoma Biblia tu na hakuna kuhubiri kwani mahubiri hayajaandikwa neno kwa neno kwenye Biblia. Tulinde Imani yetu daima.
Sala: Bwana nisaidiye niweze kulinda Imani yangu. Amina.
Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment