Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

4th APRIL 2025


 


KUWEKA MAJARIBUNI





 “KWARESIMA YA UKARIMU”
Tafakari ya Kwaresima
Ijumaa, Aprili, 4, 2025,
Juma la 4 la Kwaresima

Hek 2: 1, 12-22;
Zab 34: 17-21, 23;
Yn 7: 1-2, 10, 25-30.


KUWEKA MAJARIBUNI


Kitabu cha Hekima kina kadiriwa kuandikwa miaka mia kabla ya kuja Kristo. Lakini cha kushangaza maelezo yake yanaonekana kuwa karibu sana katika kumwelezea Yesu. Somo la leo linaongelea kuhusu mtu ambaye anamjua Mungu na hata anajiita “Mtumishi wa Mungu” (Hek 2:3). Na kama Yesu, huyu mtu ana adui ambao wanamfuatilia ili kumtega katika maneno yake na hata kutaka kumua. (2:19-20).

Leo tunakumbushwa kwamba kutakuwa na upinzani daima juu ya Kristo na wale wanao mfuata. Katika somo la Injili, tunasoma, juu ya kushindwa kwa jaribio la kumkamata Yesu wakati wa sikukuu ya Tabernaklo kwasababu “saa yake bado” (Yn 7:30). Ni kweli, Yesu alisulubiwa na kufa, lakini kifo hakikuweza kumweka chini. Mungu alimfufua! Ndivyo hivyo sisi Mungu hataruhusu kitu tunacho vumilia kituangushe bila kutusaidia. Atatuimarisha. Atatupa neema. Atatuinua tena.

Yesu anatuita sisi tuwe mabalozi wake. Anatutaka sisi tushirikishe habari njema kwa kila mtu tunae kutana naye. Huu ndio wito wa pekee, lakini pia kuna changamoto zake. Pengine juhudi zetu zitafanikiwa baada ya kupata upinzani mkubwa na majaribu makubwa, na hata changamoto nyingine ni za kusukumwa. Lakini tukibaki imara katika kushirikisha Injili kwa upendo na sio kwa kujiona wema wenyewe, kwa furaha na sio hasira, tutabarikiwa sana. Yesu atatuambia “vyema mtumwa mwema ingia katika furaha ya Bwana wako” (Mt 25:21). Hauhitaji kuwa mtu uliye bobea katika kuongea au kuwa mashuhuri katika kuongea. Wala haupaswi kuwa na nguvu labda nyingine. Tunapaswa kutambua tu Yesu anatupa nguvu na neema tunapo amua kumshuhudia. Na neema yake itatutunza kama ilivyo na nguvu ya kuwavuta watu kwake.

Sala: Bwana, nakupenda. Nisaidie nikuone na kukupenda wewe katika jirani zangu. Nisaidie ninapo wekwa katika majaribu, na familia yangu, marafiki zangu, na wengine wanao nipinga kwasababu ya kukutangaza wewe na thamani ya Injili yako. Tufariji daima tunapo tangaza Injili yako. Tupe nguvu yako ya Kimungu. Yesu nakuamini wewe. Amina

Copyright ©2013-2025 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

MASOMO YA MISA, APRILI 4, 2025






MASOMO YA MISA, APRILI 4, 2025
IJUMAA, JUMA LA 4 LA KWARESIMA


SOMO 1
Hek. 2:1, 12-22

Wasiomsadikia Mungu walisema hivi, huku wakimfikiri yasiyo kweli, Zaidi ya hayo na tumwotee mtu wa haki, maana hatuna haja naye, naye yu kinyume cha matendo yetu; atukaripia ya kama tumeiasi torati, na kutushitaki ya kama tumekosa adabu. Asema ya kwamba anamjua Mungu, na kujiita mtumishi wa Bwana. Ametuwia magombezi ya fikira zetu. Hata kumtazama twaona ni kugumu; maan amaisha yake si sawasawa na masiha ya wengine, na mwenendo wake ni wa kigeni. Tuanhesabiwa naye kuwa kama madini hafifu; anajitenga na njia zetu kama na uchafu. Wenye haki asema kuwa mwisho wao ni heri; hujivuna ya kwamba Mungu ndiye baba yake.

iwa ni mwana wa Mungu, Yeye atamtegemeza na kumwokoa mikononi mwa adui zake. Na tumhakikishe kwa jeuri na maumivu, ili tujifunze upole wake na kuithibitisha saburi yake akidhulumiwa. Hata tumhukumu auawe mauti ya aibu, maana ataangaliwa sawasawa na maneno yake.

Ndivyo walivyosemezana, wakakosea kabisa. Kwa maana uovu wao uliwapofusha; hawakuzijua siri za Mungu; wala hawakuutarajia mshahara wa utakatifu, wala kudhani ya kwamba iko thawabu kwao wenye roho zisizo na hatia.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 34:16-20, 22 (K) 18

(K) Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo.

Uso wa Bwan ani juu ya watenda mabaya,
Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
Walilia, naye Bwan akasikia,
Akawaponya na taabu zao zoe. (K)

Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo,
Na waliopondeka roho huwaokoa.
Mateso ya mwenye haki ni mengi,
Lakini Bwana humponya nayo yote. (K)

Huihifadhi mifupa yake yote,
Haukuvunjika hata mmoja.
Bwana huzikombo a nafsi za watumishi wake,
Wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao. (K)



SHANGILIO
Lk. 8:15
Heri wale walishikao neno la Mungu katika moyo wao mwema na mnyofu, na wazaao matunda katika uvumilivu.



INJILI
Yn. 7:1-2, 25-30

Baada ya hayo Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya; maana hakutaka kutembea katika Uyahudi, kwa sababu Wayahudi walikuw awakitafuta kumwua.

Na sikukuu ya Wayahudi, Sikukuu ya Vibanda, ilikuwa karibu. Hata ndugu zake walipokwisha kukwea kuiendea sikukuu, ndipo yeye naye laipokwea, si kwa wazi bali kana kwamba kwa siri.

Basi baadhi ya watu wa yerusalemu wakasema, Je! Huyu siye wanayemtafuta ili wamwue? Na kumbe! Anena waziwazi, wala hawamwambii neno! Yamkini hao wakuu tuna jua hakika ya kuwa huyu ndiye Kristo? Lakini huyu twamjua atokako; bali Kristo atakapokuja hakuna ajuaye atokako.

Basi Yesu akapaza sauti yake hekaluni, akifundisha na kusema, Mimi mnanijua, na huko nitokako mnakujua; wala sikuja kwa nafsi yangu; ila yeye aliyenipeleka ni wa kweli, msiyemjua ninyi. Mimi namjua, kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma.

Basi wakatafuta kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake ili kumshika, kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 2025, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

3rd APRIL 2025





 

SALA ZINATUBADILI, TUNAKUWA VYOMBO VYA HURUMA YA MUNGU!




“KWARESIMA YA UKARIMU”
Tafakari ya Kwaresima
Alhamisi, Aprili 3, 2025.
Juma la 4 la Kwaresima

Kut 32: 7-14;
Zab 106: 19-23;
Yn 5: 31-47.


SALA ZINATUBADILI, TUNAKUWA VYOMBO VYA HURUMA YA MUNGU!

Leo somo la kwanza linatuletea swali la kushangaza. Mungu amekasirika, akiwa tayari kuwaangamiza Waisraeli kwasababu ya kuabudu miungu mingine. Lakini Musa, anaongea naye kuhusu uamuzi wake. Tunaweza kushangazwa inawezekana je Mungu wa milele asiye badilika abadili mawazo yake. Ni kitu ambacho tunaweza tusielewe. Ambacho tunaweza kusema kwa ujasiri ni kwamba Maandiko yanatupa ujumbe baada ya ujumbe ukielezea nguvu ya sala. Abrahamu aliongea na Mungu ili asiangamize mji mzima, kama kutakuwa na watu wachache wenye haki, je, kuna watu wachache kati yetu wanaoweza kusali kama Abraham kwa Mungu?

Kazi alizozitenda Yesu zilimpa ushuhuda wa utume aliopewa na Baba yake Mbinguni. Ujumbe wake uliongea na watu jinsi Baba alivyo. Ushuhuda wake ulifunua kiini cha muunganiko wake na Mapenzi ya Baba. Ingawaje miujiza yake ilikuwa ya hali ya juu kwa wote waliokuwa tayari kumwamini, kazi alioifanya ya “pekee” ilikuwa juu ya unyenyekevu na upendo wa kweli. Yesu alikuwa mwaminifu, mnyofu wa moyo kabisa. Kwahiyo, ushuhuda wa matendo yake ya kawaida ya upendo, kujali, na kufundisha ndiyo yalio ziteka na kupata mioyo ya watu wengi. Hata tendo dogo la Upendo liliongea mengi katika mioyo ya watu.

Tutafakari leo, kama tupo tayari kufuata mfano wa Musa na kuwa na muda wa kumfahamu Mungu na kuwa karibu kwa jinsi anavyo tupenda sisi. Je tupo tayari kufungua mioyo yetu kwake ili tuweze kupata huruma yake? Je, tupo tayari kwenda nje kwa wengine ambao hawana bahati kama sisi, ili tuweze kugusa mioyo yao kwa moyo wa Kimungu, kwa kuangalia mahitaji yao? Tutafakari pia wito wetu wakutoa ushuhuda wa Baba yetu wa Mbinguni, kushirikisha upendo wa Baba kwa kila tunaye kutana naye. Kama tutakumbatia utume huu, Injili itafunuliwa kwa wengine kupitia sisi, na mapenzi ya Mungu yatafunuliwa na kutimia katika ulimwengu wetu.

Sala: Bwana, ninaomba niweze kuwa shahidi wa upendo wako utokao moyoni mwako. Nipe neema niweze kuwa mkweli na mwaminifu. Nisaidie mimi niweze kuwa chombo cha uhakika cha huruma ya moyo wako ili kazi zangu zote zishuhudie huruma yako. Yesu, nakumini wewe. Amina.

Copyright ©2013-2025 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

MASOMO YA MISA, APRILI 3, 2025




MASOMO YA MISA, APRILI 3, 2025
ALHAMISI, JUMA LA 4 LA KWARESIMA

SOMO 1
Kut. 32:7-14

Bwana akamwambia Musa, Haya! Shuka kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao, wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia kuyeyusha, wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri. Tena Bwana akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu; basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize; nami ninakufanya wewe uwe taifa kuu.

Musa akamsihi sana Bwana, Mungu wake, na kusema, Bwana, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu? Kwa nini Wamisri kunena, wakisema, Amewatoa kwa kuwatenda uovu, ilia pate kuwaua milimani, na kuwaondoa watoke juu ya uso wa nchi? Geuka katika hasira yako kali, ughairi uovu huu ulio nao juu ya watu wako. Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu, nao watairithi milele. Na Bwana akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 106:19-23 (K) 4

(K) Ee Bwana unikumbuke mimi, kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako.

Walifanya ndama huko Horebu,
Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka.
Wakaubadili utukufu wao
Kuwa mfano wa ng’ombe mla majani. (K)

Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu,
Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu.
Wakamsahau Mungu, mwokozi wao,
Aliyetenda makuu katika Misri. (K)

Akasema ya kuwa atawaangamiza,
Kama Musa, mteule wake, asingalisimama,
Mbele zake kama mahali palipobomoka,
Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu. (K)



SHANGILIO
Mt. 4:17

Tubuni, asema Bwana, kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.



INJILI
Yn. 5:31-47

Yesu aliwambia Wayahudi: Mimi nikijishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli. Yuko mwingine anayeshuhudia; nami najua ya kuwa ushuhuda wake anaonishuhudia ni kweli. Ninyi mlituma watu kwa Yohane, naye akaishuhudia kweli. Lakini mimi siupokei ushuhuda kwa wanadamu; walakini ninasema haya ili ninyi mpate kuokoka. Yeye alikuwa taa iwakayo na kung’aa, nanyi mlipenda kuishangilia nuru yake kwa muda.

Lakini ushuhuda nilio nao mimi ni mkubwa kuliko ule wa Yohane; kwa kuwa zile kazi alizonipa Baba ili nizimalize, kazi hizo zenyewe ninazozitenda, zanishuhudia ya kwamba Baba amenituma. Naye Baba aliyenipeleka amenishuhudia. Sauti yake hamkuisikia wakati wowote, wala sura yake hamkuiona. Wala neno lake hamnalo likikaa ndani yenu, kwa kuwa ninyi hammwamini yule aliyetumwa na yeye.
Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia. Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima. Mimi siupokei utukufu kwa wanadamu. Walakini nimewajua ninyi ya kuwa hamna upendo wa Mungu ndani yenu. Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, wala ninyi hamnipokei; mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea huyo.

Mwawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamwutafuti? Msidhani kwamba mimi nitawashitaki kwa Baba; yuko anayewashitaki, ndiye Musa, mnayemtumaini ninyi. Kwa maana kama mngalimwamini Musa, mngeniamini mimi; kwa sababu yeye aliandika habari zangu. Lakini msipoyaamini maandiko yake, mtayaamini wapi maneno yangu?

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 2025, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

2nd APRIL 2025


 

FURAHI KATIKA MAPENZI YA MUNGU!




“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Kwaresima
Jumatano, Aprili 2, 2025. 
Juma la 4 la Kwaresima

Isa 49: 8-15;
Zab 145: 8-9, 13-14, 17-18;
Yn 5:17-30


FURAHI KATIKA MAPENZI YA MUNGU!

Kama mtoto wa Yosefu mseremala, alijifunza ni nini baba yake alipenda. Muda baada ya muda alikuja kuelewa zaidi, jinsi ya kunyoosha au kukata vipande viwili na kuviunganisha. Alianza kuona kazi iliomalizika ya baba yake, kuona meza au kiti alicho tengeneza baba yake. Na mwisho pengine aliweza kutengeneza kama baba yake na kumfanya baba yake afurahi. Leo katika Injili Yesu anaongea na Baba yake wa Mbinguni katika hali ya mfanano kama hiyo. Anasema na kufanya yale malengo ya Baba yake. Kwasababu ameyaweka malengo yote moyoni mwake. Anatambua kabisa katika hali zote ni kwa ajili ya ukombozi. 

Kwa upande wetu, tunaweza kuchukua uelewa wa umoja huu wa Baba na Mwana, somo la utukufu jinsi ya kuingia katika umoja huu na Mungu. Pili, tunapaswa kuamini tunacho elewa, na tukichague kwa ajili ya maisha yetu. Changamoto ni kwamba kuna sauti nyingi zinazo tuita na kushindana na maamuzi yetu. Tukiwa tunachagua kati ya hizo, kuchagua tu ile ambayo Mungu anatufunulia, tunakuwa tunavutwa moja kwa moja kwa mapenzi ya Mungu na kuyafanya. Kwa njia hii sisi nasi tunakuwa wamoja na Mungu. 

Kama Yesu, sisi wote tunataka kufanya mapenzi ya Mungu. Lakini ili kuwa wenye mafanikio katika kazi zetu tunapaswa kutambua picha yote. Mara nyingi tunachoka tukijaribu kuchagua vitu vidogo, kwamba sijui Mungu atapenda nibaki katika familia yangu jioni hii au niende kwenye mkutano parokiani. Ni wazi Yesu anajali kila kitu katika maisha yetu, lakini tutajikuta ni rahisi kufanya uchaguzi sahihi wakati tukiwa na uelewa mkubwa juu ya nini Baba anatengeneza na ni kwa jinsi ghani anatualika kila mmoja wetu kuingia katika malengo yake makubwa. 

Sala: Baba wa Mbinguni, ninakushukuru kwa zawadi ya Yesu Mwanao na ninakushukuru kwa umoja mlionao. Nivute katika utukufu uliopo katika kuyafanya mapenzi yako. Nifanye mmoja wako, uendelee kuwa Baba yangu daima. Baba wa Mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, nakuamini wewe. Amina .

Copyright ©2013-2025 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

MASOMO YA MISA, APRILI 2, 2025





MASOMO YA MISA, APRILI 2, 2025
JUMATANO: JUMA LA 4 LA KWARESIMA

SOMO 1
Isa. 49:8-15

Bwana asema hivi, Wakati uliokubalika nimekujibu, na siku ya wokovu nimekusaidia; nami nitakuhifadhi, nitakutoa uwe agano la watu hawa, ili kuiinua nchi hii, na kuwarithisha urithi uliokuwa ukiwa; kuwaambia waliofungwa, Haya, tokeni; na hao walio katika giza, Jionyesheni.

Watajilisha katika njia, na juu ya majabali watapata malisho. Hawataona njaa, wala hawataona kiu; hari haitawapiga, wala jua; kwa maana yeye aliyewarehemu atawatangulia, naam, karibu na chemchemi za maji atawaongoza. Nami nitafanya milima yangu yote kuwa njia, na njia kuu zangu zitatukuzwa zote.

Tazama, hawa watakuja kutoka mbali; na tazama, hawa kutoka kaskazini, na kutoka magharibi, na hawa kutoka nchi ya sinimu. Imbeni, enyi mbingu; ufurahi, Ee nchi; pazeni sauti ya kuimba, enyi milima; kwa kuwa Bwana amewafariji watu wake, naye atawahurumia watu wake walioteswa.

Bali Sayuni alisema, Yehova ameniacha, Bwana amenisahau. Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 145:8-9, 13-14, 17-18 (K)

(K) Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma.

Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma,
Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema.
Bwana ni mwema kwa watu wote,
Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote. (K)

Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
Ni mamlaka yako ni ya vizazi vyote.
Bwana huwategemeza wote waangukao,
Huwainua wote walioinama chini. (K)

Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,
Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote.
Bwana yu karibu na wote wamwitao,
Wote wamwitao kwa uaminifu. (K)


SHANGILIO
Mt. 4:4

Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.


INJILI
Yn. 5:17-30

Yesu aliwajibu Wayahudi: Baba yangu anatenda kazi hata sasa, nami ninatenda kazi. Basi kwa sababu hiyo Wayahudi walizidi kutaka kumwua, kwa kuwa hakuivunja sabato tu, bali pamoja na hayo alimwita Mungu Baba yake, akijifanya sawa na Mungu.

Basi Yesu akajibu, akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile. Kwa kuwa Baba ampenda Mwana, naye humwonyesha yote ayatendayo mwenyewe; hata na kazi kubwa zaidi kuliko hizi atamwonyesha ili ninyi mpate kustaajabu. Maana kama Baba awafufuavyo wafu na kuwahuisha, vivyo hivyo na Mwana ahuisha wale awatakao. Tena Baba hamhukumu mtu yeyote, bali amempa Mwana hukumu yote, ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka.

Amin, amin, nawaambia, yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani. Amin, amin, nawaambia, Saa inakuja, na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai.

Maana kam avile Baba alivyo na uzima nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na uzima nafsini mwake. Naye akampa amri ya kufanya hukumu kwa sababu ni Mwana wa Adamu. Msistaajabie maneno hayo; kwa maana sasa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu. Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenipeleka.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 2025, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.