MASOMO YA MISA JUNI 5, 2026
ALHAMISI, JUMA LA 9 LA MWAKA
KUMBUKUMBU YA MTAKATIFU BONIFASI, ASKOFU NE MFIADINI
SOMO 1
2 Tim. 3 :10-17
Wewe umeyafuata mafundisho yangu, na mwenendo wangu, na makusudi yangu, na imani, na uvumilivu, na upendo, na saburi; tena na adha zangu na mateso, mambo yaliyonipata katika Antiokia, katika Ikonio, na katika Listra, kila namna ya adha niliyoistahimili; naye Bwana aliniokoa katika hayo yote. Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa. Lakini watu wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika.
Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, Iafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 119 : 157, 160-161, 165-166, 168 (K) 165
(K) Wana amani nyingi waipendao sheria yako.
Wanaonifuatia na watesi wangu ni wengi,
lakini sikujiepusha na shuhuda zako.
Jumla ya neno lako ni kweli,
na kila hukumu ya haki yako ni ya milele. (K)
Wakuu wameniudhi bure,
ila moyo wangu unayahofia maneno yako.
Wana amani nyingi waipendao sheria yako,
wala hawana la kuwakwaza. (K)
Ee Bwana, nimeungojea wokovu wako,
na maagizo yako nimeyatenda.
Nimeyashika mauasi yako na shuhuda zako,
maana njia zangu zote zi mbele zako. (K)
SHANGILIO
Zab. 111 :7, 8
Aleluya, aleluya, Maagizo yako yote, ee Bwana, ni amini, yamethibitika milele na milele. Aleluya.
INJILI
Mk. 12:35-37
Yesu alipokuwa akifundisha katika hekalu, alijibu, akasema, Husemaje waandishi ya kwamba Kristo ni Mwana wa Daudi? Daudi mwenyewe alisema, kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, hata niwawekapo adui zako kuwa chini ya miguu yako. Daudi mwenyewe asema ni Bwana; basi amekuwaje mwanawe? Na mkutano mkubwa walikuwa wakimsikiliza kwa furaha.
No comments:
Post a Comment