Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JANUARI 29, 2026


 


MASOMO YA MISA, JANUARI 29, 2026 ALHAMISI, JUMA LA 3 LA MWAKA SOMO 1 2 Sam. 7:18-19, 24-29 Daudi, mfalme, aliingia, akaketi mbele za Bwana, akasema, Mimi ni nani, Bwana Mungu, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta hata hapa? Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Ee Bwana Mungu; hata umeleta habari ya nyumba yangu mimi, mtumwa wako, kwa miaka mingi inayokuja baadaye; na hayo kwa namna ya kibinadamu, Ee Bwana Mungu. Nawe ulijifanyia imara watu wako Israeli, wawe watu wako milele; nawe, Bwana, umekuwa Mungu wao.
Basi sasa, Ee Bwana Mungu, neno lile ulilolinena katika habari za mtumwa wako, na katika habari za nyumba yangu, ulifanye imara milele, ukatende kama ulivyosema. Jina lako na litukuzwe milele, kusema, Bwana wa majeshi ndiye Mungu juu ya Israeli; na nyumba ya mtumwa wako, Daudi, itakuwa imara mbele zako. Kwa kuwa wewe, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, umenifunulia mimi, mtumwa wako, ukisema, Nitakujengea nyumba; kwa hiyo mimi, mtumwa wako, nimeona vema moyoni mwangu nikuombe dua hii. Na sasa, Ee Bwana Mungu, wewe ndiwe Mungu, na maneno yako ndiyo kweli, nawe umemwahidia mtumwa wako jambo hili jema; basi, sasa, uwe radhi, ukaibarikie nyumba ya mtumwa wako, ipate kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, Ee Bwana Mungu, umelinena; na kwa Baraka yako nyumba ya mtumwa wako na ibarikiwe milele. Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI Zab. 132:1-5, 11-14 (K) Lk. 1:32 (K) Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, Baba yake. Bwana, umkumbukie Daudi Na taabu zake zote alizotaabika. Ndiye aliyemwapia Bwana, Akaweka nadhiri kwa shujaa wa Yakobo. (K) Sitaingia hemani mwa nyumba yangu, wala sitapanda matandiko ya kitanda changu; sitaacha macho yangu kuwa na usingizi wala kope zangu kusinzia, hata nitakapompatia Bwana mahali, na shujaa wa Yakobo maskani (K) Bwana amemwapia Daudi neno la kweli, hatarudi nyuma akalihalifu, baadhi ya wazao wa wmili wako nitawaweka katika kiti chako cha enzi. (K) Wanao wakiyashika maagano yangu, na shuhuda nitakazowafundisha, watoto wao nao wataketi katika kiti chako cha enzi milele. (K) Kwa kuwa Bwana ameichagua Sayuni, ameitamani akae ndani yake. Hapo ndipo mahali pangu pa raha milele, Hapo nitakaa kwa maana nimepatamani. (K)
SHANGILIO Zab. 119:105 Aleluya, aleluya, Neno lako ni taa ya miguu yangu, ee Bwana, na mwanga wa njia yangu. Aleluya. INJILI Mk. 4:21-25 Yesu aliwaambia wafuasi wake: Mwaonaje? Taa huja ili kuwekwa chini ya pishi, au mvunguni? Si kuwekwa juu ya kiango? Kwa maana hakuna neno lililositirika, ila makusudi lije likadhihirika; wala hakuna lililofichwa, ila makusudi lije likatokea wazi. Mtu akiwa na masikio ya kusikia, na asikie. Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa. Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa. Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo Copyright © 2026, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

No comments:

Post a Comment