Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA OKTOBA 29, 2025

 


MASOMO YA MISA OKTOBA 29, 2025
JUMATANO, JUMA LA 30 LA MWAKA
_____________

SOMO 1
Rum 8:26-30

Roho hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu. Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 13: 3-6

(K) Nimezitumainia fadhili zano, Ee Bwana. 

Ee Bwana, Mungu wangu, uangalie, uniitikie;
Uyatie nuru macho yangu,
Nisije nikalala usingizi wa mauti.
Adui yangu asije akasema, Nimemshinda;
Watesi wangu wasifurahi ninapoondoshwa. (K) 


Nami nimezitumainia fadhili zako;
Moyo wangu na uufurahie wokovu wako.
Naam, nimwimbie Bwana,
Kwa kuwa amenitendea kwa ukarimu. (K)


SHANGILIO
1Sam. 3:9 

Aleluya, aleluya,
Nena Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia, wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya.



INJILI
Lk. 13: 22-30

Yesu alikuwa akipita katika miji na vijiji, akifundisha, katika safari yake kwenda Yerusalemu. Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaokolewa katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia wasiweze.

Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako; ndipo mtakapoanza kusmea, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu. Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu.

Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje. Nao watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu.

Na tazama, wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
_____________

Copyright © 2025, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment