MASOMO YA MISA, FEBRUARI 26, 2025
JUMATANO, JUMA LA 7 LA MWAKA
SOMO 1
YbS. 4:11-19
Hekima huwafundisha wanawe na kuwaelimisha wanaomsikiliza. Wao wampendao hupenda uzima, nao wamtafutao watapata kibali kwa Bwana. Wao wamshikao wataurithi utukufu, hata na kudumu katika baraka ya Bwana. Wao nao wamtumikiao watamhudumia yeye aliye Mtakatifu, nao wampendao Bwana huwapenda. Amsikiaye atahukumu kwa kweli, naye amjalie atakaa katika chumba chake cha ndani. Akimtumaini atamrithi, atakuwa naye hata vizazi vyote vya milele. Kwa maana mwanzo Hekima ataandamana naye kwa njia za kikombo, na kumletea hofu na woga, na kumwadhibisha kwa marudi yake, hata atakapoweza kumwamini roho yake, na kumhakiki kwa hukumu zake. Ndipo atakaporudi na kumuongoza moja kwa moja, na kumfurahisha, na kumfunulia siri zake. Walakini akipotea, Hekima atamwacha na kumtia mikononi mwa maangamizi.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab 119:165, 168,171-172, 174-175
(K) Wana amani nyingi, ee Bwana, waipendao sheria yako.
Wana amani nyingi waipendao sheria yako,
Wala hawana la kuwakwaza. (K)
Nimeyashika mausia yako na shuhuda zako,
Maana njia zangu zote zi mbele zako. (K)
Midomo yangu na itoe sifa,
Kwa kuwa unanifundisha mausia yako. (K)
Ulimi wangu na uiimbe ahadi yako,
Maana maagizo yako yote ni ya haki. (K)
Ee Bwana, nimeutamani wokovu wako,
Na sheria yako ndiyo furaha yangu. (K)
Nafsi yangu na iishi, ipate kukusifu,
Na hukumu zako zinisaidie. (K)
SHANGILIO
Aleluya, aleluya,
Maagizo yako yote, ee Bwana, ni ambayo yamethibitika milele na milele.
Aleluya.
INJILI
Mk 9:38-40
Yohane alimjibu Yesu, akamwambia, Mwalimu, tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi. Yesu akasema, Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya; kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2025, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment