Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, OKTOBA 10, 2025


MASOMO YA MISA, OKTOBA 10, 2025

IJUMAA, JUMA LA 27 LA MWAKA
________
SOMO LA 1
Yoe 1:13-15; 2:1-2

Jikazeni mkaomboleze enyi makuhani; pigeni yowe enyi wahudumu wa madhabahu; Njoni mlale usiku kucha katika magunia, Enyi wahudumu wa Mungu wangu; Kwa kuwa sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji zimezuiwa katika nyumba ya Mungu wenu. Takaseni saumu, iteni kusanyiko la dini, Wazee na wakusanye wenyeji wote wa nchi; waende nyumbani kwa Bwana, Mungu wenu na kumlilia Bwana, Ole wake siku hii! Kwa maana siku ya Bwana inakaribia, nayo itakuja kama uangamivu utokao kwake aliye mwenyezi. Pigeni tarumbeta katika Sioni, pigeni na kelele katika mlima wangu mtakatifu; wenyeji wote wa nchi na watetemeke; kwa maana siku ya Bwana inakuja. Kwa sababu inakaribia. Siku ya giza na weusi, siku ya mawingu na giza kuu. Kama mapambazuko yakitandazwa juu ya milima, hao ni wakuu, tena wenye nguvu, mfano wao haukuwako kamwe, wala hautakuwako baada ya hao, hata katika miaka ya vizazi vingi.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
________
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 9:1-2.5.15.7-8

(K) Bwana atauhukumu ulimwengu kwa haki.

Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote;
Nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu;
Nitafurahi na kukushangilia Wewe;
Nitaliimbia jina lako, Wewe uliye juu. 

Umewakemea mataifa;
Na kumwangamiza mdhalimu;
Umelifuta jina lao milele na milele;
Mataifa wamezama katika shimo walilolifanya;
Kwa wavu waliouficha imenaswa miguu yao.

Bali Bwana atakaa milele, 
Ameweka kiti chake tayari kwa hukumu.
Naye atauhukumu ulimwengu kwa haki;
Atawaamua watu kwa adili.
________
SHANGILIO
1Thes. 2:13

Aleluya, aleluya,
Lipokeeni neno la Mungu, siyo kama neno la wanadamu, 
bali kama neno la Mungu.
Aleluya.
________
INJILI
Lk. 11:15-26

Wengine wa makutano walisema, Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo. Wengine walimjaribu, wakitaka ishara itokayo mbinguni. Naye akajua mawazo yao, akawaambia. Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka. Basi, ikiwa shetani naye amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa kuwa ninyi mnasema kwamba mimi natoa pepo kwa Beelzebuli. Basi, kama mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je! Huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu. Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama; lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang’anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake.

Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu aliyekusanya pamoja nami hutawanya.

Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema, Nitarudia nyumba yangu niliyotoka. Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio waovu kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
      ________

Copyright © 2025, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment