"ASALI ITOKAYO MWAMBANI"
Tafakari ya kila siku
Jumapili, Julai 16, 2023,
Juma la 15 la Mwaka
Jumapili, Julai 16, 2023,
Juma la 15 la Mwaka
Isa. 55: 10-11
Ps. 64:10-14
Rom. 8:18-23
Mt 13:1-23
MBEGU NI NENO LA MUNGU
Neno liwe, limezungumzwa au kuandikwa, lina ushawishi mkubwa kwetu sisi sote. Kwa mfano: Mwalimu anaposema kitu, wanafunzi hufanya. Wazazi wanaposema kitu, watoto hutii.wazee huzungumza na vijana, husikiliza, na kathalika. Yale tunayoyaona au kusikiliza kupitia TV, Redio au kwenye magazeti yana ushawishi mkubwa sana kwetu sote. Hakuna anayeweza kukataa hili.
Lakini swali linabaki, kama maneno ya mwanadamu, yana ushawishi mkubwa namna hiyo kwetu, je, ni kwa nini maneno ya Mungu, yanachukua muda mrefu katika kutushawishi? Au, ni kwa nini yanachukua muda mrefu, kuingia mioyoni mwa watu? Jibu linapatikana katika mfano wa mpanzi, anaoutoa Bwana Yesu katika Injili ya leo.
Katika mfano huu, Bwana Yesu anajulishwa kwetu kama mkulima, na mbegu ni neno la Mungu. Mbegu hizo, zilizoanguka kwenye njia, miamba, miiba, na penye udongo mzuri, zinawakilisha makundi ya watu wa aina mbalimbali, ambao husikiliza neno la Mungu. Wengine walilipokea hilo neno, na kulikataa mara moja. Wengine walilipokea, lakini baadaye wakalisahau, na wengine walilipokea, wakalikubali na kulistawisha. Katika makundi yote haya, neno la Mungu lilipokelewa kwa furaha, isipokuwa kundi moja tu, ambalo lililikataa mara moja. Kwa hiyo, tatizo haliko kwenye kupokea neno la Mungu, bali tatizo lipo ni jinsi gani ya kulitunza na kuliishi. Kwa hakika, tunaweza kusema kwamba, kuna hatua tatu za kulienzi neno la Mungu, ambazo ni kulipokea, kulihifadhi na kuliishi.
Hatua ya kwanza, ni kulipokea neno la Mungu, hapo ndipo akili inaposhirikishwa, hii ni kwa njia ya kusikiliza kwa makini kile kinachosemwa na kufafanuliwa.
Hatua ya pili, kulihifadhi hilo neno la Mungu hii inashirikisha moyo, ambao huangalia matumizi ya hilo neno katika maisha yetu, na jinsi gani linaweza kustawisha maisha yetu ya kila siku. Hii inatakiwa kufanyika kwa wiki nzima mara baada ya neno la jumapili.
Hatua ya tatu, ni jinsi gani ya kuliishi hilo neno la Mungu ambalo akili imelipokea na moyo kulihifadhi. Yaani, roho zetu!
Hatua zote hizi tatu, zinaweza kuelezeka kwa kusikiliza mfano ufuatao. Kuna hadithi inayomuhusu mtu mmoja aliyeitwa Ndg. Bill, ambaye alikuwa ni Contracta wa kudumu. Katika muda Fulani, hali ya biashara yake ilimfanya awe mlevi. Hivyo, alifilisika kibiashara na kutengana na familia yake. Siku moja, alipokuwa anatembea mitaani, aliona msumari wenye kutu na uliojikunja. Bill aliwaza moyoni mwake ‘maisha yangu ni kama huu msumari! Mimi nami ninakutu na kupinda, mimi si chochote, na si lolote ni wakutupwa nje kama huu msumari’.
Lakini aliokota ule msumari na kuweka mfukoni mwake. Alipofika nyumbani alichukua nyundo na kuanza kuunyoosha na baadaye alichukua msasa na kuusugua. Halafu akachua msumari mpya na kuchanganya pamoja na ule aliouokota. Ilikuwa vigumu sana kwake kuitofautisha. Ndipo, alipoanza kuyafikiria maisha yake, kwamba yanaweza kunyoka na kutu iliyomo ikaondoka kama ule msumari. Lakini inawezekana? Je, alikuwa tayari kuvumilia mapigo ya nyundo pamoja na msasa? Aliamua kujaribu! Hivyo, alijikuta maisha yake yakibadilika na akaungana tena na familia yake na kurudi kwenye kazi yake ya ukontracta.
Katika hadithi hii, tumeona hatua tatu. Hatua ya kwanza ni ushirikishwaji wa akili, ambapo ni pale Bill, alipogundua kwamba yeye hana tofauti na ule msumari uliopinda. Hatua ya pili, ni ushirikishwaji wa moyo, ambapo Bill, aliamua kuunyoosha na kuusugua, ule msumari na kutambua kwamba yeye naye anaweza akayanyoosha maisha yake. Na hatua ya tatu, ni ushirikishwaji wa moyo/roho, ambapo Bill, anaamua kubadilisha mwendo wa maisha yake.
Kama somo la kwanza, linavyotuasa kwamba neno litazaa matunda iwapo tu tutalipokea, kuliifadhi na kuliishi. Ndw, ni rahisi kulisikiliza neno la Mungu. Lakini, je, ni rahisi kuliishi? Hivyo kama alivyofanya Bill, nasi tunaalikwa kujaribu. Kwani kwa kujaribu ndipo mabadiliko hutokea, kwa hiyo katika ibada hii tumwombe Mkombozi wa dunia Bwana Yesu, atupe neema ili tuweze kuliishi neno lake analotulisha kila siku.
Sala: Bwana nisaidie mimi niweze kuwa udongo mzuri wa neno lako. Ninakuomba nisikilize yote unayoniambia ili niweze kupanda mbegu ya imani ndani mwangu. Ninakuomba Imani hii ikuwe na kuleta Baraka unazotaka. Yesu nakuamini wewe. Amina
Copyright ©2013-2023 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment