Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, DESEMBA 17, 2022

 

MASOMO YA MISA, DESEMBA 17, 2022

Jumamosi ya 3 ya Majilio


SOMO 1
Mwa 49:2, 8-10

Yakobo akawaita wanawe akawaambia; Kusanyikeni, msikie, enyi wana wa Yakobo, Msikilizeni Israeli, baba yenu. Yuda, ndugu zako watakusifu, Mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako. Wana wa baba yako watakuinamia. Yuda ni mwana-simba, Kutoka katika mawindo, mwanangu, umepanda; Aliinama akajilaza kama simba, Na kama simba mke; ni nani atakaye mwamsha? Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii.


WIMBO WA KATIKATI
Zab 72:1-4, 7-8, 17

(K) Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.

Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako,
Na mwana wa mfalme haki yako.
Atawaamua watu wako kwa haki,
Na watu wako walioonewa kwa hukumu. (K) 

Milima itawazalia watu amani,
Na vilima navyo kwa haki.
Atawahukumu walioonewa wa watu,
Atawaokoa wahitaji, (K) 

Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi,
Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.
Na awe na enzi toka bahari hata bahari,
Toka Mto hata miisho ya dunia. (K)

Jina lake na lidumu milele,
Pindi ling'aapo jua jina lake liwe na wazao;
Mataifa yote na wajibariki katika yeye, Na kumwita heri. (K) 


SHANGILIO

Aleluya, aleluya,
Ee Hekima ya Aliye juu, unayepanga yote kwa nguvu zako na utaratibu mwema, uje kutufunza njia ya busara.
Aleluya.


INJILI
Mt 1:1-17

Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu. Ibrahimu alimzaa Isaka; Isaka akamzaa Yakobo; Yakobo akamzaa Yuda na ndugu zake; Yuda akamzaa Peresi na Zera kwa Tamari; Peresi akamzaa Esromu; Esromu akamzaa Aramu; Aramu akamzaa Aminadabu; Aminadabu akamzaa Nashoni; Nashoni akamzaa Salmoni; Salmoni akamzaa Boazi kwa Rahabu; Boazi akamzaa Obedi kwa Ruthu; Obedi akamzaa Yese; Yese akamzaa mfalme Daudi. Sulemani akamzaa Rehoboamu; Rehoboamu akamzaa Abiya; Abiya akamzaa Asa; Asa akamzaa Yehoshafati; Yehoshafati akamzaa Yoramu; Yoramu akamzaa Uzia; Uzia akamzaa Yothamu; Yothamu akamzaa Ahazi; Ahazi akamzaa Hezekia; Hezekia akamzaa Manase; Manase akamzaa Amoni; Amoni akamzaa Yosia; Yosia akamzaa Yekonia na ndugu zake, wakati wa ule uhamisho wa Babeli. Na baada ya ule uhamisho wa Babeli, Yekonia akamzaa Shealtieli; Shealtieli akamzaa Zerubabeli; Zerubabeli akamzaa Abihudi; Abihudi akamzaa Eliakimu; Eliakimu akamzaa Azori; Azori akamzaa Sadoki; Sadoki akamzaa Akimu; Akimu akamzaa Eliudi; Eliudi akamzaa Eleazari; Eleazari akamzaa Matani; Matani akamzaa Yakobo; Yakobo akamzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa YESU aitwaye Kristo. Basi vizazi vyote tangu Ibrahimu hata Daudi ni vizazi kumi na vinne; na tangu Daudi hata ule uhamisho wa Babeli ni vizazi kumi na vinne; na tangu ule uhamisho wa Babeli hata Kristo ni vizazi kumi na vinne.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment