SKAPULARI YA KARMELI
Katika barua yake, Mtakatifu Yohane Paulo II anasema: “Taratibu utajiri huu wa Wakarmeli wa kumrithi Maria umekuwa hazina ya Kanisa zima kwa sababu ya kuenea kwa desturi ya skapulari. Kwa usahili wake, kwa umuhimu wake wa kibinadamu na kwa uhusiano wake na nafasi ya Maria kuhusu Kanisa na binadamu, desturi hii ilipokelewa na taifa la Mungu kwa dhati na upana hata ikaja kutangazwa ni kumbukumbu ya tarehe 16 mwezi Julai kwenye kalenda ya liturujia ya Kanisa zima”.
SKAPULARI
Inatokana na neno la kilatini ‘Scapulae’ ambalo maana yake ni mabega. Ni vazi refu ambalo linavaliwa juu ya kanzu ya kitawa. linaangukia mbele na nyuma. Skapulari ni alama ya kuwa tayari kutumikia.
ZAWADI KUTOKA KWA BIKIRA MARIA WA MLIMA KARMELI
Tarehe 16, mwezi Julai, mwaka 1251, wakati Mtakatifu Simoni Stoki alipokuwa amezama katika sala mbele ya sanamu ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, mama Maria akiwa katika utukufu wote wa mbinguni na malaika wake alimtokea. Alikuwa, amevaa vazi la Karmeli, na katika mkono mmoja alikuwa ameshikilia Skapulari takatifu, na katika mkono mwingine alikuwa amembeba mtoto Yesu. Alimpa Mt. Simoni skaplari na kumwambia, “chukua skaplari hii ya Shirika la Karmeli mwanangu. Hii itakuwa ni ishara ya ulinzi wangu kwa shirika lote. Yeyote atakayeivaa skaplari hii na kufa akiwa ameivaa, hataonja jehanamu.”
SKAPULARI KAMA ISHARA TAKATIFU
Skapulari ni moja kati ya visakramenti kwa sababu mbili zifuatazo. Kwanza, imethibitishwa na Kanisa kwa karne kadhaa zikijumuisha hivi karibuni “Ibada ya kubariki na kuingiza watu katika Skapulari ya Bikira Maria Mbarikiwa wa Mlima Karmeli.” Pili, kwa sababu pamoja na neema zinazoendana na Skapulari, kuna wajibu pia unaotokana na kuvaa ishara hiyo ya heshima kwa Bikira Mtakatifu.
Visakramenti ni ishara takatifu zinazofanana na sakramenti kwa sababu vinadokeza matunda yake, hasa ya kiroho, ambayo yanapatikana kwa maombezi ya sala ya Kanisa. Kanisa lina nguvu ya pekee, kwa sababu ni ni mchumba mtakatifu na safi wa Kristo. Visakramenti ni tofauti na sakramenti kwa vile viko vingi, vimewekwa na Kanisa, na zinazaa matunda yake si kama sakramenti ambazo zinatenda kwa kufanyika tu (ex opere operato - maana yake si kwa nguvu ya stahili binafsi za yule anayezitoa au anayezipokea) bali kwa maombezi ya Kanisa.
ISHARA YA SKAPULARI
Ili tuweze kupata uelewa wa asili wa maana ya kidini ya Skapulari ya Karmeli inatubidi kwanza kuelewa umbile na maana ya alama na ishara katika mchakato mzima wa ujuzi na mawasiliano, katika nyanja zote mbili za maisha ya kawaida na yale yapitayo maumbile. Maisha ya kawaida ya binadamu yamejaa ishara na alama hasa katika uwanja wa mawasiliano. Mwanga mwekundu ni ishara ya onyo mbele ya hatari; kinyume chake, mwanga wa kijani unaonyesha hali ya usalama. Mwanga, moto, maji n.k., ni ishara zinazoashiria mambo mengi, ya kawaida na yapitayo maumbile. Kama ishara ya urafiki huwa tunashiriki mlo wa pamoja, kama ishara ya mshikamano tunashirikiana katika mgomo, kama ishara ya utambulisho wetu tunaungana kusherehekea sikukuu ya Taifa. Heshima kwa bendera ni kielelezo na ishara ya uaminifu kwa nchi yetu.
Tunatumia ishara nyingi kuashiria mambo ya kiroho na hata yale yapitayo maumbile. Yesu ndiye ishara na zawadi kuu ya upendo wa Baba. Yeye alianzisha Kanisa kama ishara na chombo cha upendo wake. Yesu alitumia mkate, divai na maji, kutusaidia tuelewe mambo ya juu zaidi ambayo hatuwezi kuyaona walakuyagusa . Katika adhimisho la Ekaristi na Sakramenti nyingine ( Ubatizo, Kipaimara, Upatanisho, Ndoa, Daraja takatifu, Mpako wa wagonjwa) alama zote (maji, mafuta, kuwekea mikono, pete na vazi la harusi) zina maana yake maalumu na zinatuwezesha kuwasiliana na Mungu aliyemo ndani ya vitu hivyo. Ni ishara wazi ya mambo yasiyoonekana. Licha ya alama hizo za kiliturujia, Kanisa linazo nyingine zinazohusiana na baadhi ya matukio, mapokeo au watu. Mojawapo kati ya hizo ni Skapulari ya Kahawia ya Karmeli.
Papa Yohane Paulo II anaeleza hivi thamani ya ishara ya Skapulari: “Kwa hiyo kuna kweli mbili zinazoliliwa kwa ishara ya Skapulari: upande mmoja ulinzi wa daima wa Bikira Mwenye heri, si tu katika safari ya maisha, lakini pia wakati wa kuvukia ukamilifu wa utukufu wa milele; upande mwingine ujuzi wa kwamba heshima kwake haiwezi kuishia sala na sifa katika nafasi fulanifulani, bali inatakiwa kuwa aina ya vazi, yaani iwe dira ya kudumukatika mwenendo wetu wa Kikristo kwa mfumo wa sala na maisha ya kiroho, kwa njia ya kupokea mara nyingi sakramenti na kwa kutekeleza matendo ya huruma ya kiroho na ya kimwili. Kwa njia hiyo Skapulari inakuwa ishara ya ‘agano’na uhusiano kati ya Maria na mwumini. Hakika inathibitisha ile zawadi aliyotupa Yesu msalabani yaani Mamaye ambaye alimkabidhi kwa Yohane na kwa njia yake kwetu sisi sote, pamoja na kumkabidhi Maria huyo mtume mpendwa na sisi pia awe Mama yetu wa kiroho”. Hivyo Skapulari ni ishara ya nje inayoonyesha kuwa sisi ni watoto wa Maria na kwamba tunafanya kila tuwezalo ili kuvaa maadili yake tuweze kurudisha ulimwenguni mwanga wa uzuri wa utakatifu wake . Inadhihirisha upendo na ulinzi wa Maria na uwajibikaji wake wa kimama kwetu sisi sote. Yeye anatufundisha kuwa kama Yesu, ambaye ndiye njia ya kwenda kwa Baba. Maria anaongozana nasi ili tuitikie kama yeye : “Nitendewe kama ulivyonena.” Skapulari ni ishara ya ulinzi wa upendo wake kwetu sisi tunapojaribu kuwa waaminifu kwa Mwanae. Inatukumbusha kuiga fadhila zake za imani, upendo, unyenyekevu n.k. Inatuasa kukimbilia sala hata kuzamia mafumbo. Ni ishara ya uwepo wake wa kimama kwetu. Inatuhimiza kutafakari daima neno la Mungu. Inatufanya tuwe karibu na mahitaji ya watu, inatusaidia kumtambua Mungu aliyemo katika yote yanayotokea kandokando yetu.
SALA
Mama Maria Mlima wa Karmeli, Mama yetu, utufunike kwa vazi la ulinzi wako wa pekee, ili tukiwa tumefunikwa na vazi lako tuweze kuletwa kwa Yesu Kristo, ambaye tunaishi katika agano naye. Amina
BAADHI YA KANUNI ZA KUFUATA
Watu huingizwa kwenye Skapulari mara moja tu na Padre au mtu yeyote aliyepewa ruhusa. Hapo baadaye badala ya Skapulari inaweza kutumika nishani yenye upande mmoja picha ya Moyo Mtakatifu wa Yesu na upande mwingine picha ya Maria. Skapulari inatutaka tuishi kama Wakristo hasa kwa kufuata mafundisho ya Injili, tupokee sakramenti, tukiri heshima yetu ya pekee kwa Bikira Mwenye heri, ambayo inapaswa kuonyeshwa kila siku, walau kwa kusali Salamu Maria mara tatu.
Pokea Skapulari hii, ishara ya uhusiano wako wa pekee na Maria Mama wa Yesu ambaye unaahidi kufuata mfano wake. Iwe kwako ukumbusho wa hadhi yako kama Mkristo katika kuhudumia wengine na kumwiga Maria. Ivae kama ishara ya ulinzi wake na ya ushirika wako katika familia ya Karmeli ukifanya mapenzi ya Mungu na kujitolea kujenga ulimwengu unaolingana na mpango wake wa ushirikiano, haki na amani.
Copyright ©2022 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment