Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

Lengo la Daudi lilikuwa ni kumfundisha mtoto wake

 *ASALI MUBASHARA-Jumanne 01/02/2022*


Karibuni sana ndugu wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza mfalme Daudi anapokea habari za kifo cha mtoto wake Absalomu. Huyu alikuwa mtoto mtukutu aliyetaka kumwua baba yake, yaani mfalme Daudi na kuchukua madaraka.


Daudi anapopokea habari ya kifo chake, anasikitika, anaumia kwa kifo chake japokuwa Absalomu ndiye aliyekuwa akitafuta uhai wa babaye, lakini Daudi anahuzunika kwa ajili ya uhai wa mwanae. Kwa hakika ndugu zangu Daudi alijua yote kuhusu ujinga wa Absalomu kwamba alikuwa mtoto mwenye tamaa, na alisikitika namna jinsi tamaa zake zilivyokuwa zinampeleka pabaya. Lengo la Daudi lilikuwa ni kumfundisha mtoto wake, amfundishe atambue maisha yalivyo lakini nafasi kama hii haikupatikana, alifariki kabla ya Daudi kumpatia somo. 


Sisi ndugu zangu tumwige mfalme Daudi. Tujue kwamba wapo wenzetu wenye kuongozwa na roho za kishetani, wenye kupenda tamaa tamaa na kujiamini kupita kiasi. Wanangangania mambo wasiyoyaweza kwa wakati wote. Wapo watu wa namna hii na lengo letu liwe ni kwa ajili ya sisi kuwafundisha na sio kuwalipa kadiri ya tamaa zao. Tuwe na moyo wa kuwafundisha zaidi kama Daudi alivyopendelea kumfundisha mtoto wake Absalomu. 


Katika somo la injili, Yesu anakwenda kumponya mtoto wa Afisa Jairo na anapokuwa njiani, anakuwa tayari kumponya mama mwenye ugonjwa wa kutokwa na damu. Mama aliyemgusa Yesu njiani alikuwa na matatizo makubwa lakini alijipa moyo. Hali yake ya ugonjwa ya kutokwa na damu kuendana na sheria za kiyahudi alipaswa asijichanganye kwenye kundi kubwa la watu kwani angaliwanajisi. Lakini Yeye mwenyewe anajipa moyo, anaondoa hofu yote, ananyanyuka na kumtafuta Yesu. Kwa hakika katika kumfuata Yesu, lazima tujipe moyo, tuondokane na hofu, lazima tunyanyuke sisi kama sisi kwani sisi ndio wenye shida na kukumbana na Yesu mwenyewe atakayekuwa msaada wetu.


Tusitegemee kwamba yupo mwingine atakayemgusa Yesu kwa ajili yetu kwani sisi ni sisi na wao ni wao. Sisi ndio wenye kutambua magumu na maumivu yetu. Tumguse Yesu sisi kama sisi. Tumsifu Yesu Kristo.

No comments:

Post a Comment