Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

KUWA WATU WASIO NA HILA!

 

“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”

Alhamisi, Januari 6, 2022,

Juma kabla ya Epifania

 

1Yoh. 4:19-5:4

Zab. 72:1-2, 14-15 (K) 11

Lk. 4:14-22

 

 

KUWA WATU WASIO NA HILA!

Ndugu zangu wapendwa, karibuni kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza Mt. Yohane anazidi kusisitiza juu ya upendo kwamba huo ndio utambulisho, amri kuu aliyopewa Mkristo. Hivyo ahakikishe kwamba anaitii na kuitimiza. Mt. Yohane anaendelea kusema kwamba hakuna awezaye kusema kwamba anampenda Mungu halafu na hapohapo anamchukia ndugu yake. Hii ndivyo kanuni ilivyo kwa sababu huu ni unafiki, kujipendekeza kwa Mungu lakini huwapendi watoto wake, kwani Mungu huonekana kupitia watoto wake tunaokutana nao kila siku.

Somo hili linatuchoma wengi wetu. Kwa sababu hatuna upendo wa dhati, hata tutoapo misaada tunakuwa na malengo yetu binafsi, tunatoa pale tunapojua kwamba tutapokea baadaye. Hatupo tayari kutoa pale tusipopokea. Pia tunatabia ya kutoa kujitafutia jina na umaarufu. Mara nyingi hatutoi misaada sehemu ambayo hatuonekani, au kutambuliwa. Tutatoa pale tunapoonekana tu. Na pia tunatabia ya kutangaza tulichotoa. Tuachane na tabia za namna hii ndugu yangu.

Siku ya leo tujichunguze na kuona ni yupi tunayekosana naye, tusimchukie yeyote. Wote ni watoto wa Mungu. Tutambue kwamba wanadamu sio malaika, tusitegemee wawe kamili katika kila hali. Basi, tuwapokee katika udhaifu wao. tusimchukie yeyote.

Yesu katika somo la injili anajitokeza katika nguvu ya Roho Mtakatifu na kuanza kuhubiri habari njema. Anapata kuwatangazia watu wa kijijini kwake kwamba Roho wa Bwana yu juu yake na kwa njia ya Roho huyu anaweza kutangaza uhuru kwa wafungwa na watumwa wengi. Sisi tuombe kuwa na Roho huyu. Roho atatupatia mawazo mapya ya kufanya shuhguli zetu. Atatupatia maneno yenye hekima ya kuwashauri wenzetu. Pia atafanya vichwa vyetu na mioyo yetu vifikirie mawazo yenye tija kuliko mawazo ya kushindwa shindwa kila wakati. Hakika atatupatia ukombozi toka katika udhaifu wetu. hivyo, tumwombe Mungu siku ya leo atupe Roho huyu.

Copyright ©2013-20202 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

 

No comments:

Post a Comment