“ASALI ITOKAYO
MWAMBANI”
Jumatatu, Januari 10,
2022
Juma la 1 la Mwaka.
1Sam. 1:1-8
Zab. 116:12-14, 17-19
(K)
Mk. 1:14-20
KUISIKILIZA SAUTI YA
MUNGU!
Karibuni sana wapendwa
wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika
somo la injili, Bwana Yesu anaanza utume wake hadharani. Hii ni baada ya Yohane
kutiwa Gerezani.
Sijui Yohane alijisikia
vipi, yaani baada ya kufanya kazi yote kubwa hii, baada ya kumbatiza Yesu na
kumtambulisha machoni pa wote, Yohane anaishia gerezani. Inaonekana kwamba
Yohane kama Nabii aliendelea kumtumainia Mwenyezi Mungu. Lakini ndivyo hali
ilivyo, mara nyingi, mtu mwema ndiye anayedhulumiwa kuliko alivyo mwovu. Hata
mti mzuri hutupiwa mawe mengi zaidi kuliko ilivyo miti mingine mibaya kama vile
miiba.
Sisi tuwe tayari
kuvumilia pale tunapomfuata Bwana. Yesu anapoanza utume wake, ujumbe anaoanza
nao ni wa kutubu na kuiamini injili. Huu ndio utakaoiokoa dunia. Duniani dhambi
nyingi zinatendeka na madhara ya dhambi ya mmoja huwafikia wengi kwani duniani
tunaishia kwenye jamii na kosa la mmoja huiadhiri dunia nzima. Hivyo, tunapaswa
kuomba msamaha hata kwa ajili ya makosa yasiyotendwa na sisi.
Yesu anapoendela na
utume wake, anawaita wafuasi wake na kuwaahidi kuwa wavuvi wa watu zaidi kuliko
wa samaki. Mwanadamu ni kiumbe kikuu kuliko viumbe vingine. Hivyo, kuwa mvuvi
wake ni miongoni mwa heshima kubwa mwanadamu anaweza kupewa. Hii yaashiria
kwamba lengo la Yesu ni kutukabidhi vitu vyema.
Sisi ndio wenye
kujichagulia vitu visivyo na thamani na kudhania kwamba ni vyenye thamani.
Tujifunze kutafuta yaliyo ya thamani toka kwa Bwana. Tunyanyuke na kumfuata
Yesu nasi tutaonyeshwa ya thamani. Tutatumia muda wetu kwa ajili ya thamani.
Tutafanya ya thamani na kujifunza ya thamani.
Katika somo la kwanza,
Hanna, atakayekuja kuwa mama yake Samweli, anaonekana kudharaulika machoni pa
Penina, aliye mke mwenza. Hanna ataendelea kumlilia Mungu na Mungu atampatia
mtoto, tena atakayekuja kuisaidia Israeli kwa muda mrefu sana. Hakika Mungu ana
mipango yake. Na pale anapoichelewesha, jua kwamba kuna mambo mazuri anataka
yatokee na mambo mazuri hayahitaji haraka.
Mwanadamu anapaswa kuwa
mvumilivu pale anaposubiri haya yaliyo mazuri. Asiwe na moyo wa papara na Bwana
kwa hakika atamsaidia tu. Uvumilivu ni mlango wa kutufungulia kuyapata yaliyo
makubwa na mazuri zaidi. Tuombe kuwa wavumilivu.
Copyright
©2013-20202 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment