Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

WOTE WANAALIKWA KWENYE MEZA YA YESU!

 

“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”

Ijumaa, Desemba 10, 2021,

Juma la 2 la Majilio

 

Isa 48:17-19;

Zab 1:1-4, 6;

Mt 11:16-19

 

 

WOTE WANAALIKWA KWENYE MEZA YA YESU!

Ndugu zangu karibuni kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Katika somo la kwanza Nabii Isaya anawakumbusha wana wa Yuda kwamba dhambi na ukaidi wao ndio uliowasababishia hasara, fedheha na maumivu yote waliyoyapata utumwani. Hivyo, anawataka wasirudie tena ukaidi wao ili wabarikiwe na Bwana.

Katika injili ya leo, Yesu anasikitishwa tena na ukaidi wa Wayahudi. Yeye alijitahidi kujishusha, akashiriki maisha yao, kula na kunywa pamoja nao, akashiriki pia shida zao ili apate kuwaonea huruma na kuwaongoa wengi (Ebr 4:14-16). Lakini wakamdhihaki na kumtukana kama mdhambi kama Babu zao walivyoyakataa mafundisho ya manabii. Hapa Yesu anawaonya na kuwaambia kwamba wasipomsikiliza yeye mwishowe kitawapata kama kile kilichowapata Babu zao.

Sisi Wakristo ni Israeli mpya. Tusipuuzie unabii wowote alioutoa Yesu au unaotolewa na wafuasi wake yaani kanisa. Tuuheshimu ili mwishoni kisije kikatupata kilichowapata Wayahudi katika uhamisho.

Mafarisayo pia walimuonea Yesu wivu kwasababu alikuwa maarufu sana kuliko wao, hivyo waliogopa kupoteza umaarufu wao na hivyo kuanza kumtungia vitu vya uongo, ati, ni mlafi na nk. Nasi kwa hofu ya kupoteza umaarufu wetu tunaweza kuwazushia watu uongo ili sisi tupendwe na kuonekana wazuri zaidi, au tupewe sifa zaidi, lazima tuwe makini tukubali viaji na mapaji aliowajalia Mungu watu wengine.

Tuna bahati ya kuhubiriwa ujumbe wa Neno la Mungu kila siku zaidi sana hata kwenye mitandao, tusipo angalia vizuri, tunaweza kuchagua tu vile vitu tunavyopenda kusikia, tena kama vinagusa maisha yetu tunajifanya hatuoni na mwishowe, kuishia kuwa kama Mafarisayo. Tukaribishe unabii wa Neno la Mungu hata kama linauma, kubali likuchome ili uanze maisha mapya. Tumuombe Yesu tukisema, Ee Yesu unijalie neema ya kutambua nguvu iliyoko katika unabii wa Neno lako ili nisije hata mara moja nikapuuzia unabii mtakatifu. Amina!

 

Copyright ©2013-2020 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment