Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

Sisi tujifunze toka kwa Yosefu.

 

“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”

Jumamosi, Desemba 19, 2021,

Juma la 3 la Majilio

 

Yer. 23:5-8

Zab. 72:1-2, 12-13, 18-19 (K) 7

Mt. 1:18:24

 

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika Zaburi ya wimbo wa katikati linatupatia matumaini ya ujio utakaoleta furaha na amani milele. Mwenyehaki anatangazwa kwamba ndiye atakayesitawi na kupata amani yake milele.

Mungu ndiye mwenye uwezo wa kuleta amani na furaha kwa milele yote. Na kwa hakika Zaburi hii ilikuwa utabiri wa ujio utakaokamilisha hili. Yesu ndiye ukamilifu wa unabii huu.

Katika somo la kwanza, Yeremia anatutangazia kwamba Yesu ndiye chipukizi toka katika shina la Daudi, atakayetenda kwa hekima, na kutoa hukumu ya haki. Yuda anayeonewa na mataifa ataokolewa. Nabii kwa hakika anaufurahia ujio huu kwa namna ya pekee. Yesu ndiye ukamilifu wa yote yanayotangazwa na nabii leo.

Hivyo tujifunze kumwamini Yesu. Kwa hakika yeye ndiye mfalme wetu, ndiye mwenye kutupa faraja yetu, ndiye mwalimu wetu. Ulimwengu wote, viongozi wote wa ulimwengu wanapaswa kujifunza toka kwa Yesu. Wajifunze kuwa watu wa haki na kutawala kwa amani. Tabia za unganganiaji wa madaraka, ubinafsi na rushwa vinaleta maumivu kwa wengi na vita duniani na yote haya ni kwa sababu tumekataa kumwiga Yesu kama Mfalme na mwalimu wetu. Yesu ndiye mwalimu. Tujifunze kumtii mfalme na mwalimu huyu.

Katika somo la Injili, tunapata habari za kuzaliwa kwa Yesu. Kuzaliwa huku hakukuwa rahisi sana kwani Yosefu na Maria walikuwa bado hawajapata uelewa wa kutosha kuhusu kuzaliwa huku. Yosefu anakusudia kumwacha Maria kwa siri. Malaika wa Mungu anamfumbulia Yosefu fumbo lililojificha kati yao na mwishowe Yosefu anakubali kumpokea Yesu na Maria.

Sisi tujifunze toka kwa Yosefu. Ukweli ni kwamba familia nyingi zina changamoto lakini tujifunze kumsikiliza malaika wa Bwana ambaye huja na kusema nasi kila siku akitufundisha namna ya kutatua hizo changamoto kama anavyomfundisha Yosefu leo. Wengi wetu hatuisikilizi sauti ya Bwana kama alivyofanya Yosefu. Tunaenda kuomba ushauri kwa watu wavijiweni na wanatupatia ushauri mmbaya na mwishowe tunaharibu familia. Tuombe ushauri kwa watu wanaosali na waliokaribu na Bwana hakika watatuongoza vyema. Tumsifu Yesu Kristo.

 

Copyright ©2013-2020 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

 

 

No comments:

Post a Comment