“MBEGU ZA UZIMA”
JUMAPILI, DESEMBA 5, 2021.
------------------------------------------------
DOMINIKA YA 2 YA MAJILIO
Somo la 1: Bar 5: 1-9, Nabii Baruku anaona maono juu ya uhuru wa watu wake ambao wapo utumwani wakati ambapo Mungu atawarudisha Yerusalemu kwa furaha na mwanga wa utukufu wake.
Wimbo wa Katikati: Zab 125, Utuokoe Ee Bwana katika utumwa wetu, kama vile kijito cha maji katika jangwa
Somo la 2: Flp 1: 4-6, 8-11, kiini cha somo hili ni ujumbe wa umoja, uvumilivu, kumshuhudia Yesu na Injili bila kuyumbishwa. Paulo aliandika kwa ukarimu mkubwa kwa Wafilipi, akiwahakikishia kwamba kile alicho anzisha Mungu kwa ubatizo ndani mwao atakikamilisha.
Injili: Lk 3:1-6, somo hili linatuambia juu ya kutokea kwa Yohane Mbatizaji. Kiini cha ujumbe wa Yohane ni kwamba Mungu anakuja kuwakomboa watu wake. Watu wanaalikwa kuandaa njia kwa kufanya toba.
MAJILIO: ANDAA NJIA YA BWANA
Mtu mmoja alikuwa na saa kubwa ya gharama sana iliyotengenezwa Switzerland. Aliiweka dirishani, sehemu ambayo ilionekana na wote waliokuwa wakipita njia na wengi walirekebisha majira ya saa zao kwa kutazama saa hii. Lakini siku moja saa ilipata shida Fulani. Ilianza kuonyesha saa ambayo sio. Hivyo mwenye saa kila siku alitumia nguvu nyingi na muda mwingi kuwa karibu na saa ili aiweke kwenye wakati unaotakiwa. Hali hii iliendelea kwa miaka. Siku moja mtu alimfuata akamwambia kwanini “badala ya kutumia nguvu nyingi na muda wako mwingi kuweka saa hii kwenye wakati sahihi kila siku, kwanini usirekebishe vifaa vya ndani?” Yule mwenye saa alifurahi kwani hakuwahi kufikiri hivyo. Sisi nasi tuonaogopa kubadilika kutoka ndani kwani tunaogopa kuonakana vibaya machoni pa watu au pengine tutapoteza umaarufu wetu kwasababu watu wameshatuona kama watu wenye saa ya gharama hivyo tunafanya kila jitihada umaarufu wetu usipotee, na hivyo tunateseka kweli. Kwanini tusibadilike kutoka ndani na kuanza kufurahia maisha kama yalivyo?
Mungu hakumtuma Mwanae aje abadili watu wachache. Alimtuma Mwanae awabadili watu wote na ubinadamu wote. Ndio maana kila majilio tunakutana na Yohane Mbatizaji akitutangazia ujio wa ukombozi wa wanadamu wote. Anawaambia watu “kuanda njia kwa ajili ya ujio wa Bwana”. Lakini kwanini tunahitaji kujiandaa kwa jili ya Bwana?
Siku moja mtu mmoja alivyutwa na jagi nzuri aliloona sokoni. Alilinunua na kwenda nalo nyumbani. Baada ya kuliweka sebuleni na kutazama nyumba yake alitambua kwamba lile jagi lake lilikuwa nzuri sana kuliko nyumba yake na hivyo akaamua kupaka rangi nyumba yake. Na kununua kateni nzuri za rangi zuri, na kununua makochi na kupendezesha nyumba yake. Kwa njia ya jagi lile nyumba nzima ilibadilika na kuwa nyumba mpya. Wakati Yesu anapo ingia katika maisha yetu anabadili kila ktiu. Kila kitu ambacho kinahitaji kubadilika kitaonekana dhahiri. Tunapo sogea karibu zaidi na Mungu ndivyo tunavyozidi kujiona tulivyo na kuona utofauti wetu! Na hii ndio maana tunayohitaji kuandaa njia kwa jili ya Bwana.
Majilio ni kipindi cha kungojea ujio wa Bwana, na Bwana pia anatusubiri kurudi kwetu kutoka kwenye dhambi. Mungu wetu anatupenda sisi na upendo wake unatufanya sisi tumtafute yeye. Mungu alienda kuwatafuta adamu na Eva katika bustani ya edeni, wakati wakiwa wamejificha, walijificha baada ya kujua kwamba wameenda kinyume na kazi ya Mungu. Wakati mwingine sisi tunalalamika Mungu amejificha mbali na uso wetu, na kwamba haonekana lakini katika hali ya kweli sisi ndio tuliojificha kutoka kwake? Na hivyo Mungu akauliza swali: “upo wapi” ni Mungu mwenyewe aliye anza kutafuta, kwa upendo wake kwetu. Agano lote la kale ameendelea kumtafuta Mwanadamu na kumleta kwenye upendo wake. Je, tupo tayari kumkaribsha yeye katika maisha yetu?
Katika somo la Kwanza nabii Baruku, ambaye alikuwa katibu wa nabii Yeremia. Anawafariji waisraeli kwa shairi. Sehemu ya taifa imesharudi kutoka utumwani, lakini hakuna hekalu ambalo limeshajengwa ili kumtukuza Mungu kama ilivyokuwa desturi ya Wayahudi. Ili kuwafariji watu Baruku anauita mji wao mama na malkia. Mungu ataisawazisha milima-pengine hapa alikuwa anataka kuondoa hali ya kutamani kuabudu milima kama mataifa mengine walivyokuwa wakifanya. Nakupanda miti ya kivuli katika barabara za nchi ya Israeli. Katika kiroho ni kwamba Mungu anaziangusha dhambi na kutuweka chini ya uvuli wa mbawa zake. Katika barua kwa Wafilipi, Paulo anaendeleza maada hii; “aliye anzisha kazi hiyo njema ndani mwenu yeye mwenyewe aikamilishe mpaka “Kristo atakapo kuja.”-hapa anamanisha ujio wa pili wa Kristo, na hukumu ya mwisho.
Maandalizi yetu ni muhimu tuangalie mioyo yetu na kumkaribisha Mungu katika maisha yetu, na uponyaji wake ili Roho Mrtakatifu atufanye viumbe vipya. Toba inaanza kwa kutambua umuhimu wa kumpokea Mungu, kwa kujitazama sisi ni nani na tupo kwa ajili ya nini, pia kutazama jitihada zetu za kumfuata Kristo. Ni kutambua uhaba wetu wa kiroho na kumfuata Yesu mkombozi wetu, na ambaye anatupatia nguvu ya kukuwa katika mapendo. Noeli itakosa maana kama hatutaandaa njia katika mioyo yetu kwa ajili ya Bwana. Wakati huu wa majilio, tujiulize hivi ni dhambi gani inaniweka mbali na Mungu? Tuuungame na kufanya toba ili upendo wa Mungu utukute sisi.
Sala: Ninakushukuru Bwana, kama Mchungaji mwema unatulisha sisi, unatukusanya kama Mchungaji ukituchukua kifuani pako kwa uangalifu. Njoo Bwana Yesu! Ninatamani kubaki katika mikono yako kwa milele yote. Bwana, tunaomba tuone ukarimu wako, tujalie ukombozi wako. Yesu nakuamini wewe. Amina.
No comments:
Post a Comment