MASOMO YA MISA NOVEMBA 4, 2021
ALHAMISI, JUMA LA 31 LA MWAKA
SOMO 1.
Warumi 14:7-12
Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake.
Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana.
Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia.
Lakini wewe je! Mbona wamhukumu ndugu yako? Au wewe je! Mbona wamdharau ndugu yako? Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu.
Kwa kuwa imeandikwa,
Kama niishivyo, anena Bwana, kila goti litapigwa mbele zangu;
Na kila ulimi utamkiri Mungu.
Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu.
Neno la Bwana.......Sifa kwako ee Kristo.
WIMBO WA KATIKATI
Zaburi 27:1,4,13-14 (K)13
(K)Naamini ya kuwa nitauona wema wa BWANA Katika nchi ya walio hai.
BWANA ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
BWANA ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani?
(K)
Neno Moja nimelitaka kwa BWANA,
Nalo ndilo nitakalolitafuta,
Nikae nyumbani mwa BWANA
Siku zote za maisha yangu,
Niutazame uzuri wa BWANA,
Na kutafakari hekaluni mwake.
(K)
Naamini ya kuwa nitauona wema wa BWANA
Katika nchi ya walio hai.
Umngoje BWANA, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje BWANA.
(K)
SHANGILIO.
Mathayo 11:28
Aleluia Aleluia
Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
Aleluia!
INJILI.
Luka 15:1-10
Basi watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia wamsikilize.
Mafarisayo na waandishi wakanung’unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao.
Akawaambia mfano huu, akisema,
Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone?
Naye akiisha kumwona, humweka mabegani pake akifurahi.
Na afikapo nyumbani kwake, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimekwisha kumpata kondoo wangu aliyepotea.
Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu.
Au kuna mwanamke gani mwenye shilingi kumi, akipotewa na moja, asiyewasha taa na kufagia nyumba, na kutafuta kwa bidii hata aione?
Na akiisha kuiona, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimeipata tena shilingi ile iliyonipotea.
Nawaambia, Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye.
Neno la Bwana......Sifa kwako ee Kristo.
Copyright © 2020, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment