MASOMO YA MISA OKTOBA 26, 2021
JUMANNE, JUMA LA 30 LA MWAKA
SOMO 1
Rum. 8; 18-25
Nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa
kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu. Kwa maana viumbe vyote pia
vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu. Kwa maana viumbe
vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake
yeye aliyevitiisha katika tumaini; kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa
huru na kutolewa katika utumwa wa uharibufu, hata viingie katika uhuru wa
utukufu wa watoto wa Mungu.
Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote
pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa. Wala si hivyo tu; ila
na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho, sisi pia tunaugua katika nafsi
zetu, tukikutazamia kufanywa wana, yaani, ukombozi wa mwili wetu. Kwa maana
tuliokolewa kwa taraja; lakini kitu kilichotarajiwa kikionekana, hakuna taraja
tena. Kwa maana ni nani anayekitarajia kile akionacho? Bali tukikitarajia kitu
tusichokiona, twakingojea kwa saburi.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 126 (K) 3
(K) Bwana alitutendea mambo makuu.
Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni,
Tulikuwa kama waotao ndoto.
Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko,
Na ulimi wetu kelele za furaha. (K)
Ndipo waliposema katika mataifa,
Bwana amewatendea mambo makuu.
Bwana alitutendea mambo makuu,
Tulikuwa tukifurahi. (K)
Ee Bwana, uwarejeze watu wetu
waliofungwa,
Kama vijito vya Kusini.
Wapandao kwa machozi,
Watavuna kwa kelele za furaha. (K)
Ingawa mtu anakwenda zake akilia,
Azichukuapo mbegu za kupanda.
Hakika atarudi kwa kelele za furaha,
Alichukuapo miganda yake. (K)
SHANGILIO
Yak. 1:21
Aleluya, aleluya,
Pokeeni kwa upole neno la Mungu
lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu.
Aleluya.
INJILI
Lk. 13:18-21
Yesu alisema, Ufalme wa Mungu umefanana
na nini? Nami niufananishe na nini? Umefanana na punji ya haradali aliyotwaa
mtu akaitupa katika shamba lake; ikamea, ikawa mti; ndege wa angani wakakaa
katika matawi yake.
Akasema mara ya pili, Niufananishe na
nini ufalme wa Mungu? Umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke akaisitiri ndani
ya pichi tatu za unga, hata ukachacha wote pia.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.
Copyright © 2020, "MASOMO YA
MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings
reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment