*ASALI MUBASHARA-JUMAPILI 03/10/2021*
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo basi neno la Bwana linaongozwa na zaburi ya wimbo wetu wa katikati zaburi ya 128 ambapo tunakutana na maneno kwamba Bwana atubariki siku zote za maisha yetu.
Haya ni maneno aliyoombewa Mfalme Sulemani na Baba yake Daudi wakati akikaribia mwisho wa uhai wake. Alimweleza kwamba kwa kila kitu ufanyacho, omba Baraka ya Mungu, kwani usipoipata, utakazana asubuhi na jioni lakini mambo yatakuwa bure. Utakuwa kama wale watu walioJenga ule mnara wa Babeli bila Baraka ya Mungu wakaishia kubomoa bila kujenga. Ndivyo ilivyo usipoomba Baraka ya Mungu.
Anaendelea kumweleza kwamba umche Mungu, uombe Baraka yake ili pia basi uweze kuona wazao wako wakiwa wamebarikiwa kwani hiyo ndiyo baraka bora kwa mwisraeli-kuwa na wingi wa watoto, watoto watakaokutunza, na wenye msimamo. Hii ni baraka kuu kuliko zote kwa Myahudi-kuwa na uzao.
Hata leo kwa wanawake wa kiafrika-uwe tasa uone. Kwa nini?
Hii ni kwa sababu baraka ya kuwa na uzao ni miongoni mwa baraka alizopewa mwanadamu tangu mwanzo wa ulimwengu. Baada ya kuumbwa walibarikiwa na kuambiwa zaeni mkaongezeke-baraka ya kwanza. Na hawa watoto lazima wazaliwe katika muungano maalumu na unaoeleweka, yaani ndoa halali.
Hili tunaona katika somo la kwanza. Mwanadamu alipoumbwa na mwenyezi Mungu, alijikuta hana wa kufanana naye, na Mungu anaamua kumtengenezea wa kufanana naye. Huyu wa kufanana naye anamtoa katika ubavu wake kuonyesha kwamba kumbe wote ni sehemu ya mwili mmoja. Kisha anawabariki kwa kuwaambia kwamba wazae na kwa pamoja waijaze nchi na kuvitawala viumbe vyote. Mungu alijua kwamba watakapobakia katika muungano mmoja, ndipo watakavyoweza kuimiliki nchi vyema.
Sasa, vilipita vizazi vingi tangu mababu wa Israeli wakitii sheria hizi na kuwaletea mafanikio makubwa. Akina Abrahamu walikaa na wanawake tasa lakini hawakuwafukuza, waliendelea kuishi nao tu. Sasa ikafikia kipindi cha Musa, kwenye kumbukumbu la Torati 24:4, watu wakazidisha kuwa na mioyo migumu zaidi, wakakosa uvumilivu hadi Musa akaruhusu talaka. Yesu katika injili anasema hii talaka sio sahihi, ni kinyume cha amri ya Mungu kwani ni mwanadamu alikosa uvumilivu na subira; mkishafunga ndoa, mnakuwa mwili mmoja na roho mmoja, mnakamilishana ule ubavu uliokuwa umetolewa na Bwana.
Sasa, huoni kwamba kuruhusu talaka ni kukeuka hili neno la Bwana kwamba wote wanakuwa mwili mmoja kwani muungano unakamilika? Hivyo anasema yeyote aliyeoa halafu akaachana na mkewe na kuona mwingine, anafanya zinaaa kwani kwa ndoa ya kwanza, ukamilisho tayari umetokea.
Ndugu zangu, kwenye masomo haya mawili, tunajifunza yafuatayo:
Kwanza, kwa kila kitu tufanyacho, tuombe baraka ya Mungu, unaweza kukazana sana ukashindwa kusogea hata hatua moja. Angalieni waliojenga mnara wa Babeli? Au Hiel aliyekuja kuujenga ule mji wa Yeriko (1Wafalme 16:34)-hakuujenga na baraka kwani ulikuwa umelaaniwa na Yoshua (Yoshua 6:26) na hivyo alipoanza kuujenga, alipoteza mtoto wake wa kwanza na alipoukamilisha, alipoteza mtoto wake wa mwisho. Hakuomba baraka ya Mungu kwenye kuujenga, alijiona kwamba ana pesa akafanya tu, aliishia pabaya. Nasi lazima tufanye vitu kwa baraka ya Mungu. Hata kama ni kiwanja, kibariki kwanza. Hata nyumba kabla ya kuhamia huko, ibariki kwanza.
Ndoa inatoa baraka-imepewa baraka maalumu na Mungu. Kuishi bila ndoa na kuzaa watoto tu bila kuomba baraka ya Mungu unakuwa kama watu wa Babeli au huyu tajiri aliyeitwa Hiel. Unaanza bila Mungu; utafika? ni laana, pale Mungu hayupo pamoja nanyi, mnafanya uzinzi, Mungu hajabariki agano hilo. Ukiingia kwenye ndoa, ndipo Mungu anapomwagia hizo baraka zake.
Hieli ambaye alikuwa myahudi aliyejenga mji wa Yeriko kichwakichwa, alianza bila baraka ya Mungu, ule mji uliaaniwa na Yoshua, yeye akaenda kuujenga. Akaishai kupata laana ya kufiwa na watoto wake.
Baraka zinazoahidiwa na huyu mzaburi leo ni kwa wale wenye ndoa, sio wale wanaozini, hawa sio baraka zao. Wewe usikazane kufyatua watoto bila kupata hii baraka, unaweza kuwafyatua wengi kulingana na pesa zako, ukawa na pesa zako lakini ukifa na unawaacha watoto wengi, hawana malezi na wajinga au wanaotangatanga, sasa ni faida gani? Hawa watoto wa nje hamjawaona-hapa ni kufanya vitu bila baraka ya mungu, uzinzi? Sasa ni faida gani kuwa nao wengi hivyo halafu wanakuja kukosa msimamo? Wazaeni kwenye ndoa wapate baraka.
Mwanadamu ni kiumbe cha hadhi ya juu, lazima azaliwe ndani ya uhusiano unaoeleweka, hawezi kuzaliwa kwenye uhusiano ambao kesho watu wamekwishatengana tayari, hii sio hivyo, mambo hayaendi hivi. Lazima azaliwe sehemu ambayo inajulikana atakula wapi, atatunzwa na nani na hata kukitokea shida ataachiwa nani. Uhusiano zisivyo na ndoa sio rahisi kukuta hivi. Watoto wanatupwa huko, je, hii sio sahihi.
Kingine ni kwamba uzinzi wote ule ni dhambi kubwa. Hata wale watoto waliozaliwa katika uzinzi, wanakuwaga na shida fulanni. Kwa nini? Tendo la uzinzi huhusu mambo makubwa, mambo ambayo mwanadamu huzaliwa, na kama ni hivyo-ni lazima liheshimiwe, haitakiwi sisi wengine kuliingilia kama hujaoa, au kuolewa kwa sababu ikitokea mtoto kazaliwa itakuwaje? Atabarikiwa vipi, mambo yataendaje?
Tuone hili, kwenye zile familia za kiasili, waliozaliwa nje ya ndoa walipata shida sana au waliozaliwa nyumbani. Kwa sababu hawapati urithi halafu kuna zile baraka fulani fulani walifanyiwa, walikuwa hawafanyiwi, unakosa wa kukufanyia. Sasa iweje na kwetu huku turuhusu watoto kuzaliwa bila ndoa?katika uzinzi? Hatuoni hasara mbeleni?
Yesu anaendelea kusema katika injili kwamba ni kwa wale wenye akili kama watoto ndio wanaweza kuingia ufalme wa mbinguni. Wanaoweza kuyapokea mafundisho haya ndugu zangu ni kwa wale wanyenyekevu.
Kuweza kukaa na mke mmoja utaonekana kuwa mjinga mjinga. Kwa mfano, mimi kuna mambo niliyoyapenda nilipokuwa nyumbani kabla ya utawa.
Nilipendaga nitoke niwe natembea kuanzia saa kumi na mbili hadi saa moja na nisikilize Bbc. Lakini sasa nina miaka karibu 16 sijawahi kufanya hivyo kwani utawani ule ni muda wa sala. Ndivyo ulimwengu ulivyo: lakini hawa ndio wale wanaoahidiwa mengi. Na ni lazima kweli tufuate hizi ratiba kama kweli tunataka kuonekana kwamba tumekomaa-niyapende maisha yangu, wito wangu. Penda wito wako, jua mipaka yako. Ili uweze kufanya hivi, kweli lazima ujishushe kama mtoto kwani kuna watakaokucheka. Hata kule kijijini, ukionekana unarudi nyumbani mapema wanakuita ati ni mwanamke, au umepewa limbwata. Lazima uwe kama mtoto kweli.
Niwaombee baraka za Mungu wale wanaoishi kwenye ndoa. Japo bado kuna misukosuko endeleeni kubeba misalaba hiyo, kweli kufika kalvari Yesu alijikwa sana. Nanyi mtajikwaa lakini jueni lengo lenu ni kufika kalvari. Iweni wanyenyekevu kama watoto.
Nasi tuishio kwenye uhusiano uchumba sugu, jua kwamba tunajizuia kupata neema. Tujitahidi tuzibariki ndoa zetu na kupata baraka. Kuna waliokataa kufunga ndoa kwa sababu ati hawana pesa, kuna anayetaka sherehe kubwa. Jamani, kuweni kama watoto, pendeni mambo ya simple. Mimi nilipata upadre-kuna waliokuwa wanaanza kunitegea wanasema hatutamchangia, lakini nilisema hapa sipo ili nimpendezeshe mtu, Napata upadre, naingia kwenye utume.
Katika somo la pili, tunaona kwamba Yesu ndiye anayetutakatifuza, lazima twende kinyenyekevu kwake tupate kutakatifuzwa naye. Tuishi vyema maagano yetu ya ndoa naye atatutakatifuza.
©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.
No comments:
Post a Comment