“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumamosi, Octoba 30, 2021,
Juma la 30 la Mwaka wa Kanisa
Roma 11: 1-2,11-12,25-29
Lk 14: 1, 7-11
KUWA WA KWANZA!
Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya
neno la Bwana asubuhi ya leo katika adhimisho la Misa Takatifu. Zaburi yetu ya
wimbo wa katikati leo inatuambia kwamba nafsi yangu inakuonea kiu ee Bwana. Hii
kweli ni sala ya mwenye imani; aliyekwisha kuuonja wema wa Bwana na hivyo
hataki kutengwa naye kabisa.
Huyu mtu ni Paulo anavyojieleza katika
somo la kwanza. Yeye basi anatoa ushuhuda leo, kaishi hapa duniani katika
ulinzi mkali kabisa wa Mwenyezi Mungu. Imefikia mahali kuona kwamba hakuna
tofauti ya kufa na kuishi. Yote ni mamoja-hii ilikuwa ni dhihirisho kubwa la
ukuu wa imani yake. Sisi tuombe kuwa kama Paulo ndugu zangu. Ifikie mahali
tuone kwamba maisha ni Kristo, kuishi au kufa yote ni ya Mungu. Wengi
hatujafikia hii hali. Hadi ile siku ya kufa tunakuwa na hofu, tunaogopa,
tunateseka, ni dhahiri kwamba bado hatujajikabidhi mikononi mwa Mwenyezi Mungu
na ndio tunaogopa. Hata baadhi ya wazee wa miaka tisini wataogopa na mwishowe
tunakuwa katika hofu.
Tuombe Mungu leo tuachane na hofu hii,
tujikabidhi mikononi mwake Mungu. Mungu atosha kabisa.
Kwenye injili Yesu anapinga watu kukaa
kwenye viti vya mbele, kujitangazia utukufu wenyewe kabla ya watu kuwatangazia
huu utukufu, kujiita watakatifu kabla ya kutangazwa. Yesu kwa hapa anakataza
tabia ya kungangania mambo; kungangani ni dhihirisho la hofu ndani ya roho ya
mtu, dhihirisho la kukosekana kwa imani, kutokujiamini kwamba nafasi yako
itabakia na hivyo unaanza kuwahi mapema.
Lakini anayejiamini hataanza kwa kuwahi
kwani anajua kwamba nafasi yake ipo tu. Na huyu anayeanza kwa kukaa kwenye
nafasi ya mbele huishia kukosa kila kitu kwani atakapokuwa ananyanyuka kurudi,
atakuta hata ile nafasi ya nyuma imekwishachukuliwa na wengine na ataishia
kusimama. Ndivyo inavyotokea na kwetu sisi pale tunapoanza kujiita
watakatifu-tunaishia kukosa kila kitu kwani wakati tunapohukumiwa na kuambiwa
kwamba hatufai, unakuta hata ile nafasi ya kutubu haipo tena kwani muda unakuta
umekwisha na tunaishia kutupwa motoni.
Ukingangania nafasi ya mbele unaishia
kujisahau na kutoitambua hali yako na huishia kuanguka zaidi. Leo tuangalie
jinsi nafasi ya mbele inavyoangusha, jinsi ilivyotufanya tuwadharau wenzetu,
tuwanyanyase wenzetu na kusahau kutubu.
------------------------
Copyright ©2013-2020 ©FurKat,
FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment