*ASALI MUBASHARA-JUMAPILI 31/10/2021*
*TAFAKARI DOMINIKA YA 31 YA MWAKA B WA KANISA*
Karibuni ndgugu zangu kwa adhimisho la misa takatifu kwenye dominika ya leo ambayo ni Dominika ya 31 ya mwaka B wa kanisa. Ujumbe wa neno la Mungu leo unatuhimiza kwenye kumpenda Mungu, apendwe kuliko vyote kwanza.
Katika zaburi yetu ya wimbo wa katikati, Daudi anaelezea sababu za yeye kumpenda Mungu-ni kwa sababu ndiye aliyehusika naye na kutembea naye wakati wa majaribu yote. Hivyo ati kwa sasa ati labda ndio kapata ufalme, ndio kaukata halafu aingie na kwenda kumtafuta miungu mingine na kumwacha yule wa zamani aliyemtesekea anasema HAPANA! nitamwabudu Mungu wangu huyu huyu aliyenipigania.
Katika somo la kwanza, Musa anawaambia wana wa Israeli kwamba hata nyie mmepiganiwa hivyovyo. Mlikuwa utumwani-lakini hakuna Miungu iliyeona mahangaiko yenu, ni mimi tu niliyeyaona. Ni mimi tu niliyepambana na Farao, nikawavusha kwenye ile bahari, nikampatia mmisri kibano. Ni mimi niliyefanya hivyo. Hivyo Musa anawaeleza kwamba wasikilize-ni lazima wamtii Bwana kwa moyo wao wote, kwa nguvu na akili zao zote.
Na Yesu anasema kwamba hii ndiyo amri kuu. Wayahudi waliisali hii kama sala kila asubuhi akiamka. Na kabla ya kufa ilibidi aisali kama kanuni yao ya imani. Na pia waliiandika juu ya kitanda chake cha kulalia ili alalapo aitambue. Kwenye mlango wa kuingilia nyumbani mwake aliiandika ili asiisahau-kwamba Mungu ndiye aliyempigania na hivyo asimwendee mungu mwingine.
Na sisi wakristo tunayosababu ya kumpenda Mungu zaidi. Sisi tulipokuwa tunaburutwa na shetani, baada ya wazazi wetu kutenda kosa na sisi kuridhi dhambi, tulibakia katika dhambi hiyo, tukiteseka na kusumbuliwa na shetani, bila matumaini. Hakuna kamungu kingine kalichojitokeza kutusaidia. Ni BWANA tu ndiye aliyenyanyuka na kutuletea Mwanae atukomboe.
Hivyo tunayokila saababu ya kumrudishia fadhila na kumpenda kwa moyo akili na nguvu zetu zote.
Tunampenda kwa moyo na nguvu kwa kuhakikisha kwamba sala tunatulia, huu ni wakati tunaomtolea yule aliyepigana kwa ajili yetu. Wakati akitupigania, hakuna mwingine aliyekuja na hivyo basi mpatie yeye nafasi.
Waisraeli walipokuwa kwenye shida walisafiri naye. Akamkimbilia naye akamwokoa. Hivyo basi leo anasema kwamba hakika hatamuacha kamwe.
Ndugu zangu, waisraeli walitembea na hizi sheria kila mahali lakini waliishi kwenye kumdharau. Walijifungia hadi vikaratasi na kuvivaa lakini wakatenda dhambi na watu walipoona kwamba wale wafarisayo watenda dhambi ndio wanatenda uovu hivi, walikwazika. Ndivyo ilivyo na sisi ndugu zangu. Unakuta tunatukana wakati tumevaa rozari na watoto wanaona. Sasa hapa wanashindwa kuona utakatifu wa rozari-kwa nini hatuiheshimu?
Au unakuta wale wanaovaa yale mavazi majoho kama wanakwaya au katekista au mapadri na masisita tunavaa nguo hizi lakini bado unajikuta unaongea kwa dharau au uonevu mkubwa. Sasa watu wanajiuliza, je, huo utakatifu uko wapi, hata hiyo nguo uliyovaa haimpatii utakatifu? Au hata kule kuhudumu kanisani hakujampatia utakatifu? Mwishowe wanakwazika na kudharau ndugu zangu.
Mara nyingi ukishaona mtu anaacha wale marafiki wake wa mwanzo au mke wake au wazazi wake ndio mwisho wako-nakueleza. Solomoni alipofanya hivi aliishia kuanguka vibaya sana. Anayefanya hivi anakosa fadhila na Mungu hapendi.
Unadharau faraja walizokuonyesha na ndio maana Mungu hukuadhibu zaidi. Watu wanakumbuka kule utotoni jinsi walivyowahi kukusaidia au kufanya mambo pamoja-sasa Mungu anapowaona hivyo wakilalamika hakuachi-atakunyenyekesha tu-solomoni ndivyo alivyonyenyekeshwa ndugu zangu. Sisi tuwakumbuke wahenga wetu. Usimwache mzazi wako.
Lazima kumpenda jirani kama nafsi yetu. Hii ni kwa sababu katika viumbe vyote hakuna kama yeye. Ni kwa sababu Mungu naye anampenda hivyohivyo kama wewe, kampigania hivyo hivyo. Huna jinsi, mpende tu. Na mbaya zaidi unaweza ukamchukia mtu, ukawa humpendi, ukamtengenezea visa lakini ukakuta ndio anachanua zaidi.
Unasema huyu simpendi lakini unakuta Mungu anampenda, kamwagia baraka ajabu. Mungu akililiwa na kila mmoja anajibu. Cha kufanya ni kushirikiana na hiki kiumbe cha Mungu ili nawe uongeze baraka juu yako na pia akuombee kwa Mungu. Ukishindana kumchukia huyu kiumbe utajikuta unalaaniwa zaidi.
Lazima tuwapende na majirani zetu kwa sababu Mungu ni mkarimu, akishaliliwa na yeyote anajibu. Hata kama ni mdhambi vipi ni kiumbe chake na atambariki na unaweza kujikuta wewe hata ukienda kuomba kitu kwake siku moja. Hivyo mpende jirani yako ndugu yangu. Akimlilia Mungu, pia anasikilizwaga. Hivyo ni lazima apendwe.
Huyu aliambiwa kwamba hayupo mbali na ufalme wa mbinguni kumaanisha kwamba bado alihitaji kupiga hatua moja mbele ili amkumbatie Mungu moja kwa Moja. Sisi tufanye hatua hiyo. Kuna mahali tunalega lega maishani mwetu. Kwa kumpokea Yesu, hatuko mbali na ufalme huu lakini inatubidi tuongeze tena bidii kidogo. Hapa hapatoshi, tunapaswa kukazana zaidi na kumpokea Mungu maisha yako yote.
©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.
No comments:
Post a Comment