ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Alahamisi , Septemba 16
2021,
Juma la 24 la Mwaka wa
Kanisa
Karibuni sana wapendwa wa
Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana leo katika
somo la kwanza, Paulo anamwagiza Timotheo juu ya tabia za anayepaswa kuwa
mtumishi wa Bwana, askofu, lazima awe mtu mwenye tabia na maadili mema ili aweze
kulitia moyo taifa la Mungu.
Ukweli ni kwamba bila
maadili, taifa la Mungu hupotea. Wana wa Sodoma na Gomora waliangamia kwa
sababu walikosa maadili mema. Askofu anapaswa kuwa mwalimu wa maadili, ili
aiokoe jamii isiangukie katika mkondo wa kupotea na kuja kuadhibiwa kama watu
wa Sodoma na Gomorah. Hivyo tutambue nafasi ya viongozi wetu wa kanisa, na
tupokee ushauri wao pale wanapotukosoa. Lakini ugumu kanisa linalokumbana nao
ni kiburi toka kwa baadhi ya kondoo wake.
Wapo kondoo wenye
majivuno, wenye kujiona kuwa wajuaji na wasiojali. Wanajiona kujua maadili na
mafundisho kuliko hata viongozi wa kanisa wenyewe. Wanapotufundisha juu ya
kuacha uchumba sugu, juu ya kuacha uasherati, juu ya kulisaidia kanisa, wengi
wetu tunadharau na mioyo yetu haijali. Tuepukane na tabia za namna hii.
Tusifikiri kwamba kwa viongozi wetu wa kanisa kukaa kimya na kufumbia macho
maovu yetu, ndiyo hali itakuwa na amani. Ukweli ni kwamba ukikaa ndani ya jamii
ambayo hakuna anayetupinga au kutukosoa ni dalili ya uwepo wa shetani ndani ya
hiyo jamii, mwenye kutufanya tujisikie kuwa salama na huru lakini kwa kiasi
kikubwa bado tupo gizani.
Watu wa Sodoma na Gomora
waliangamia kutokana na uzembe wa namna hii. Sisi tufurahie pale tukutanapo na
watu wenye kutukosoa. Wapo wazazi, ndugu, viongozi na waalimu. Wanapotukosoa,
tusikasirike au kuanzisha kisasi nao. Tuwapokee na hakika maisha yetu
yataimarika.
Katika somo la injili,
Bwana Yesu anamuonea huruma mjane wa Naini na kumpatia uhai mtoto wake
aliyefariki. Yesu anamuonea huruma mama huyu, anahuzunishwa na machozi yake na
ukiwa wake. Hakika Yesu huona machozi na ukiwa wetu. Tukimlilia kama
alivyofanya yule mjane wa Naini hakika atatuonea huruma kama alivyoweza
kumwonea huruma mama huyu. Hivyo tusiache kupeleka huzuni zetu na masikitiko
yetu kwa Bwana Yesu. Hakika atatusikiliza kama alivyomwonea huruma na
kumsikiliza mama huyu. Nasi tumwombe apate kutuonea huruma leo. Tumsifu Yesu
Kristo.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment