Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

RUDI KWA MUNGU!

 

Tafakari ya Kila siku

Ijumaa, Oktoba 1, 2021,

Juma la 26 la Mwaka

 

Bar 1: 15-22;

Ps 78: 1-5, 8-9;

Lk 10: 13-16

 

 

RUDI KWA MUNGU!

 

 

Karibuni ndugu zangu katika adhimisho la Ekaristi takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana asubuhi ya leo tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza linalotoka katika kitabu cha Baruku. Hili somo la kwanza la leo ni sala ya Baruku aliyoiandika akiwa utumwani Babuloni. Katika sala hii ambapo ndipo lilipo somo letu la kwanza, Baruku anaungama kabisa kumwambia Mungu kwamba sisi ndio tuliofanya makosa, hatukuzitii amri zako na ndiyo maana tumeishilia utumwani katika mateso haya.

 

Hivyo, katika sala hii, anawatia moyo wale walioko utumwani kwamba mrudieni Bwana jamani na kumwomba msamaha.

 

Fundisho hili la kumrudia Bwana na kumwomba msamaha pia linasisitizwa na Yesu katika injili ya leo. Yesu anaona kwamba miji ya Bestaida na korazini ilikuwa na bahati ya kusikiliza na kuona miujiza ya Yesu lakini hawakubadilika. Hivyo anawaambia kwamba wasipobadilika hakika watakiona cha moto.

 

Hili ni fundisho kubwa sana kwetu ndugu zangu hasa sisi tunaohudhuria misa kila siku. Yatupasa kuhakikisha kwamba tunakuwa mstari wa mbele katika kubadilika, katika kuonesha kwamba wewe umeielewa injili, kwamba kuja kwako kanisani kila siku kunakubadilisha-isije ikawa kwamba wewe kila siku unakuja kanisani, unakomunika, umeingia katika vyama vyingi vya kitume-lakini ukitoka hapa kanisani-nyumbani kwako au kazini kwako au mtaani kwako hakukaliki-kuko kama Guantanamo.

 

Unanyanyasa watu, vijana wako wa kazi, unawajibu watu vibaya, unatukana matusi-ukatili kila kukicha-ukiguswa kidogo unanasa watu vibao kama mchezo. Nakwambia kama uko hivyo, afadhali wale wasiokuja kanisani na adhabu yako itakuwa kubwa. Hivyo ujio wetu kanisani utufanye tubadilike. Isije ikawa kwamba unakuja kanisani kuja kuficha uovu. Tuishi Injili kwa matendo yetu na maneno yetu. Tukumbuke maneno ya Mt.Fransisko wa Assisi kwamba "tuhubiri sana na inapobidi tutumie maneno". Mt. Fransisko wa Assis atuombee katika sikukuu yake leo. Nawatakia heri na baraka ndugu zangu wa mashirika ya Mt. Fransisko kwa sherehe ya Baba yetu wa Kiserafi.

 

------------------------

Copyright ©2013-2020 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

 

No comments:

Post a Comment